Latest Posts

CHADEMA IJITENGE NA WANAHARAKATI: MJADALA WAIBUKA KUHUSU UTU NA SIASA ZA KUSHIKA DOLA

Wadau wa siasa nchini wamekitahadharisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kujitenga na mienendo ya wanaharakati wanayoitaja kuwa inadhibitiwa na hisia za mtandaoni, ili kulinda uwezekano wake wa kuaminiwa na wapiga kura na kushika dola.

Akimulika tofauti kati ya uanaharakati na siasa za chama cha dola, msanii Ibrahim Musa maarufu kama Roma Mkatoliki ameeleza kuwa wanaharakati mara nyingi hufuata mtazamo wa “jino kwa jino” ambapo adui anapofikwa na maafa huchukulia hatua hiyo kwa hisia na hata kushangilia maafa hayo.

Kupitia andiko lake kupitia mitandao ya kijamii, Roma ameonya kuwa CHADEMA kama chama chenye ajenda ya kupinga, kukosoa, na hatimaye kushika dola hakiwezi kufuata mkondo huo wa hisia.

Roma ametahadharisha kuwa chama cha upinzani kinapaswa kujiepusha na viashiria vya ukatili kabla hata hakijashika dola, kwani mpiga kura anaweza kuingiwa na hofu na kuamua kubaki na mtawala aliyepo sasa.

“Kama unamkosoa kiongozi wa Chadema kwenye maoni kisha aka-kublock means huyo siku akiwa tu DC ukakosoa atakuweka ‘ndichi’ (ndani) masaa 72!! Ni lazima anayempinga mtawala asiwe na characters za mtawala!!”

Tahadhari hiyo inakuja katikati ya mjadala mzito ulioibuka nchini kufuatia kifo cha mume wa Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Marehemu Hafidh Ameir Hassan, aliyefariki dunia Septemba 7, 2026, katika Hospitali ya Emilio Mzena na kuzikwa siku hiyo hiyo huko Kizimkazi, Zanzibar.

Wakati vyama vingine vya siasa vikienda msibani na kumfariji Rais Samia, viongozi wa CHADEMA hawakuonekana msibani wala chama kutoa taarifa rasmi ya rambirambi. Hata hivyo, Septemba 7, 2026, Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini na kukaa mahabusu kwa takribani mwaka mmoja na miezi sita, alisikika akiwaambia viongozi wake Mahakama Kuu Dar es Salaam: “Nasikia kuna msiba, wape pole… jamani pelekeni pole zangu kwa wafiwa”.

Septemba 11, 2026, kabla ya kesi yake kuanza, Lissu alisikika akirejea salamu hizo na kuhoji kama zimefika alipomuuliza Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Said Mzee: “Makamu umepeleka rambirambi zangu bwana?”, na alipojibiwa kuwa zimefika, Lissu aliongeza: “Nimefurahi kama zimefika”.

Septemba 13, 2026, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Godbless Lema, alichapisha ujumbe kwenye mitandao ya kijamii kuwasilisha salamu alizozitaja kuwa ni za Lissu na zake mwenyewe, jambo ambalo liliwawasha baadhi ya wanaharakati na wafuasi wa mtandaoni waliomshambulia Lema kwa matusi na kumwita msaliti. Wapo waliohoji ni kwanini ampe pole Rais wakati kuna watu walikufa au kuumizwa bila kupewa pole huku wengine wakidai kuwa hakuna mahali Lissu alipoashiria salamu na pole zake zilimlenga Dkt. Samia. Hata hivyo, baadhi ya wananchi walimuunga mkono Lema na Lissu kwa kile walichokiita kuonesha ukomavu wa hali ya juu.

Akijibu mashambulizi hayo Septemba 14, 2026, Lema amesisitiza kuwa hatua ya Lissu kutoa rambirambi si unyonge bali ni hekima na ukomavu akiandika, “Nimeona matusi na sintofahamu nyingi mtandaoni baada ya kuchapisha ujumbe wa kutoa pole kwa Mama Samia, hasa niliponukuu salamu za pole za Mwenyekiti Lissu kutoka gerezani. Kwa sisi jamii tunaodai kupigania uhuru wa maoni na demokrasia, hili linapaswa kutufikirisha. Kutofautiana kwa hoja hakuhitaji matusi, dhihaka wala chuki”

Naye mwanahabari Stanslaus Lambart ameeleza kuwa siasa lazima ziende na utu na kwamba Lissu na Lema walitumia nafasi hiyo kutuma ujumbe wa ubinadamu kwa washindani wao huku naye akitoa tahadhari kwa viongozi wa CHADEMA dhidi ya kutekwa na uanaharakati wa mtandaoni.

“Moja kitu kitakachoiumiza CHADEMA ni kuruhusu wanaharakati kuendesha siasa kwa shinikizo la mtandaoni (mob psychology) badala ya stadi za kisiasa zenye mikakati, diplomasia, na wakati mwingine lugha za staha hata kwa adui. Lakini mwanaharakati yeye anataka kila kitu kiwe cha ‘kupigana au kufa’ bila kuiachia akili nafasi”, ameandika Lambart na kuongeza,

“Ukiniambia niishauri CHADEMA, nitawaambia wajikite kwenye misingi ya siasa na wasikubali kuendeshwa kwa hofu ya nini kitasemwa X (Twitter) au Instagram na wanaharakati, otherwise itapoteza muelekeo”.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!