Latest Posts

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YASITISHA LESENI YA KIPE ADVENTURES KWA TUHUMA ZA UTAPELI

Wizara ya Maliasili na Utalii imesitisha kwa muda Leseni ya Biashara ya Utalii (TTBL) Na. 035388 inayomilikiwa na Kampuni ya Kipe Adventures and Safari, baada ya kupokea malalamiko mazito dhidi ya kampuni hiyo inayomilikiwa na Kipelyani Mkare Olesisian.

​Kwa mujibu wa Taarifa kwa Umma iliyotolewa leo, Oktoba 02, 2026, na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini ndani ya Wizara hiyo, hatua hiyo imechukuliwa kufuatia kampuni hiyo kupokea fedha kutoka kwa watalii wa nje ya nchi lakini ikashindwa kuwalipa watoa huduma nchini, wakiwemo wamiliki wa huduma za malazi. Kitendo hicho kiliwalazimu wageni hao kuingia gharama za ziada wakati wakiwa kwenye safari zao nchini.

​Wizara imeeleza kuwa usitishaji huo wa muda umezingatia masharti ya Sheria ya Utalii, Sura ya 65, pamoja na kanuni na masharti ya leseni hiyo, ili kutoa nafasi ya kupata maelezo ya kina kutoka kwa uongozi wa Kampuni ya Kipe Adventures and Safari.

​Kufuatia tukio hilo, Wizara imetoa rai kwa wadau wa utalii na umma kwa ujumla kuhakikisha wanahifadhi kumbukumbu zote za malipo, kuthibitisha kwa watoa huduma za malazi ikiwa nafasi zao (bookings) zimelipiwa kikamilifu, na kujiridhisha kuwa mawakala wanaowatumia wana leseni halali kabla ya kufanya malipo yoyote.

​Hali kadhalika, Wizara imewataka watalii wote walioathirika pamoja na watoa huduma wanaoidai kampuni hiyo kuwasilisha malalamiko yao kwa maandishi, yakiambatana na nyaraka au vielelezo vya madai yao, kwenda Wizara ya Maliasili na Utalii au mamlaka husika kwa hatua zaidi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!