
Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, amesema ujenzi wa Bwawa la Kidunda mkoani Morogoro ni mradi wa kimkakati utakaomaliza kabisa changamoto ya uhaba wa maji katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro, ikiwa ni utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo kuelekea 2050.
Mhandisi Kundo ametoa kauli hiyo leo Oktoba 03, 2026 wakati alipofanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Bwawa la Kidunda, lililopo Ngerengere mkoani Morogoro.
Amesema kuwa mradi huo unaogharimu Shilingi bilioni 336 zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, umefikia asilimia 70 ya utekelezaji wake.
“Bwawa hili ni suluhisho la kudumu. Litahifadhi lita bilioni 190 za maji na kuhakikisha mitambo yetu ya Ruvu Juu na Ruvu Chini inapata maji muda wote hata wakati wa kiangazi, ambapo zaidi ya wananchi milioni saba watanufaika,” amesema Mhandisi Kundo.
Amefafanua kuwa kati ya maji yatakayotolewa kwa siku, lita milioni 600 zitaelekezwa kwa DAWASA, lita milioni 400 kwa mashamba ya sukari ya Mkulazi, huku zaidi ya lita milioni 900 zikiendelea kutiririka mtoni kulinda ikolojia na mazingira katika ukanda huo.
Aidha, Mhandisi Kundo Mathew ameongeza kuwa bwawa hilo linaakisi utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuwa litazalisha megawati 20 za umeme ambazo zitaingia kwenye Gridi ya Taifa kupitia njia ya umeme ya zaidi ya kilometa 100 kutoka Kidunda hadi Chalinze, pamoja na kufungua fursa za kilimo cha umwagiliaji, uvuvi na utalii.
“Mradi huu ulisuasua tangu mwaka 1961, lakini kutokana na dhamira ya Rais Samia, leo tunaona ujenzi ukiendelea usiku na mchana. Hii ndio maana ya uchumi wa maji tulioupanga kwenye Dira ya 2050,” amesema Mhandisi Kundo.
Mhandisi Kundo amewataka wakandarasi wa mradi huo, unaosimamiwa na Bodi ya Maji Bonde la Wami-Ruvu, kuhakikisha ubora wa kazi na kukamilisha mradi kwa wakati kama ilivyopangwa, kwa sababu Serikali inatoa fedha nyingi ili kuukamilisha.