Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linatarajia kufunga transfoma mpya yenye uwezo wa MVA 120 katika Kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Dege, Kigamboni, hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa umeme na kukidhi mahitaji yanayoongezeka.
Transfoma hiyo imewasili eneo la mradi wa upanuzi wa kituo hicho wenye thamani ya Shilingi bilioni 17, unaotekelezwa na Serikali kupitia TANESCO. Awali, kituo hicho kilikuwa na transfoma yenye uwezo wa MVA 60.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa TANESCO Wilaya ya Kimbiji, Mhandisi Lukaluka Kapinga amesema ongezeko hilo la uwezo linatarajiwa kupunguza changamoto za umeme na kuboresha huduma kwa wakazi, wafanyabiashara na taasisi za Kigamboni.

Kwa upande wake, Meneja wa mradi huo, Mhandisi Edward Ngalamika, amesema utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 79.3, huku ufungaji na majaribio ya transfoma yakitarajiwa kukamilika Desemba 22, 2026.
Ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha miundombinu ya umeme na kuongeza uwezo wa kukidhi mahitaji yanayochochewa na ukuaji wa makazi na shughuli za kiuchumi Kigamboni.
