Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma wametakiwa kuhakikisha wanashiriki katika siasa safi katika maeneo yao, huku wakijikita pia katika kujenga uchumi wa chama na wa mtu mmoja mmoja.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa vibanda 20 vya biashara vyenye thamani ya shilingi milioni 100, vilivyopo Kata ya Mshangano, Manispaa ya Songea, Novemba 3, 2026, mlezi wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma, Hamad Chande, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, amesema bila uchumi thabiti hakuna siasa. Hivyo, amewataka wanachama wa CCM Mkoa wa Ruvuma kuhakikisha wanaendesha siasa safi katika maeneo yao, sambamba na kushiriki katika kujenga uchumi wa chama na uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho amesema chama hicho kinatekeleza maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuhakikisha kinabuni vyanzo mbalimbali vya mapato kupitia maeneo yanayomilikiwa na chama hicho. Amesema uwepo wa miradi katika maeneo ya chama unaongeza fursa za ajira kwa vijana wa Mkoa wa Ruvuma na kusaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana.
Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma, Mohamed Aly, amesema hadi sasa eneo la Mshangano lina jumla ya vibanda 90 vya biashara, ambapo vibanda 20 vimezinduliwa rasmi. Ameongeza kuwa katika eneo hilo pia kuna mpango wa kujenga jengo la ghorofa litakalotumika kuwa ofisi ya Chama Cha Mapinduzi Manispaa ya Songea.
