Latest Posts

SINTOFAHAMU NA SIMANZI WHITE HOUSE: MATOKEO MABAYA YA MIDTERM ELECTIONS YAZUA MSUKOSUKO UTANGAZAJI WA TRUMP

Hali ya sintofahamu imeripotiwa kutawala ndani ya Ikulu ya Marekani, White House, baada ya Rais Donald Trump kukabiliwa na matokeo mabaya ya uchaguzi wa katikati ya muhula (Midterm Elections), yaliyokipa chama cha Democratic udhibiti wa Baraza la Wawakilishi na Seneti.

Taarifa zilizochapishwa na vyombo vya habari vya kimataifa zinaeleza kuwa Trump alitumia muda mwingi wa usiku wa uchaguzi akiwa katika makazi yake binafsi ndani ya Ikulu, huku akikataa kushuka na kuungana na viongozi waandamizi wa utawala wake waliokuwa wamekusanyika katika ukumbi wa East Room kufuatilia matokeo.

Kwa mujibu wa vyanzo vilivyonukuliwa na vyombo hivyo, rais huyo alikuwa pamoja na Mkuu wa Watumishi wa Ikulu, Susie Wiles, na msaidizi wake wa karibu, Natalie Harp, wakifuatilia matangazo ya televisheni ya Fox News.

Kadiri matokeo yalivyoendelea kuonyesha ushindi wa Democratic katika majimbo mbalimbali, hali ya sherehe iliyokuwa imeandaliwa Ikulu iligeuka kuwa mazingira ya kukata tamaa, huku baadhi ya maofisa waandamizi wakiondoka kabla shughuli hiyo haijamalizika.

Taarifa hiyo inadai kuwa baadhi ya viongozi waandamizi wa serikali, akiwamo Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio, walionekana mwanzoni mwa mkusanyiko huo lakini baadaye hawakuwepo tena.

Hata vyakula vilivyoandaliwa kwa ajili ya wageni vilibaki mezani bila kuguswa, huku baadhi ya wafanyakazi wakiondoka kwenda katika maeneo ya starehe jijini Washington kujadili hatima yao ndani ya utawala huo.

Trump aelekeza lawama kwa Fox News na viongozi wa Republican

Kwa mujibu wa vyanzo vilivyonukuliwa, kufikia saa tano usiku kwa saa za Washington, Trump alikuwa amenyamaza kwa muda mrefu huku akiendelea kufuatilia matokeo kupitia Fox News.

Chanzo kimoja kilicho karibu na Trump kilieleza kuwa alikuwa amezama katika ukimya wa hasira, huku taarifa nyingine ikieleza kuwa mazingira ndani ya makazi yake yalikuwa ya huzuni na mvutano.

Hata hivyo, ukimya wake mbele ya watu haukumzuia kutoa malalamiko kupitia mtandao wake wa Truth Social.

Trump alielekeza lawama kwa Fox News, akidai kuwa mtandao huo ulichangia kushindwa kwa Republican kupitia namna ulivyoendesha matangazo na maswali ya kura za maoni za wapiga kura waliokuwa wakitoka kupiga kura.

Pia, aliikosoa hali ya kisiasa katika jimbo la Texas, akimtaja Gavana Greg Abbott katika ujumbe wake, licha ya kuwa awali alikuwa amempongeza na kumuunga mkono.

Katika ujumbe mwingine, Trump alisisitiza kuwa kama yeye angekuwa kwenye karatasi ya kupigia kura, chama chake kingeshinda kwa kishindo.

Kauli hizo zinaonyesha namna ambavyo Trump alivyokuwa akijibu matokeo yaliyokuwa yakizidi kuonyesha kupotea kwa ushawishi wa Republican katika maeneo ambayo kwa muda mrefu yalikuwa yakiiunga mkono.

Susie Wiles akabiliwa na maswali kuhusu nafasi yake

Miongoni mwa watu ambao mustakabali wao unatajwa kuwa katika mashaka ni Susie Wiles, Mkuu wa Watumishi wa Ikulu na mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa katika utawala wa Trump.

Wiles alikuwa msimamizi muhimu wa kampeni ya ushindi wa Trump katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2024 na amekuwa sehemu ya watu wa karibu wanaoratibu shughuli za kisiasa na kiutawala za Rais.

Hata hivyo, chanzo kimoja cha ndani kilichonukuliwa na vyombo hivyo vya habari vilidai kuwa Wiles alikuwa akiwahakikishia watu wa karibu na Trump kwamba Republican ingefanya vizuri katika uchaguzi huo.

Inadaiwa kuwa katika mikutano ya kila wiki iliyokuwa ikifanyika siku za Alhamisi, mshauri wa kisiasa, Chris LaCivita alikuwa akitoa matumaini kuhusu ushindi wa chama hicho.

Lakini, matokeo yalipoanza kuonyesha mwelekeo tofauti, baadhi ya watu ndani ya utawala walionekana kuanza kuhoji ufanisi wa mikakati iliyokuwa ikisimamiwa na timu hiyo.

Chanzo kimoja kilitumia neno la Kiingereza “delusional” kuelezea namna baadhi ya viongozi walivyokuwa na matumaini makubwa ya ushindi hata wakati dalili za kisiasa zilipoanza kuonyesha hali tofauti.

Hata hivyo, madai hayo ni maelezo ya vyanzo visivyotajwa majina na hayajathibitishwa kuwa msimamo rasmi wa Ikulu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!