Latest Posts

MAGONJWA MENGI YA KUAMBUKIZA YANA ASILI YA WANYAMA-PROF.KABUDI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema takwimu za kimataifa zinaonesha kuwa asilimia 60 ya magonjwa yanayoambukizwa kwa binadamu yanaweza kusambazwa kutoka kwa wanyama, huku asilimia 75 ya magonjwa mapya yakiwa na asili ya wanyama.

Kutokana na hali hiyo, Prof. Kabudi ametoa wito wa kuimarisha ushirikiano katika tafiti, kinga na udhibiti wa magonjwa yanayotokana na wanyama ili kulinda afya ya jamii na kuzuia kuenea kwa magonjwa hayo.

Amesema juhudi hizo ni muhimu pia katika kuongeza tija kwenye sekta ya mifugo pamoja na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Prof. Kabudi ameyasema hayo katika hafla ya kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya mafunzo ya Tiba ya Wanyama nchini, yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), mkoani Morogoro.

Naye Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Philip Mpango, ameiomba Serikali, kwa kushirikiana na sekta binafsi, kuongeza fedha za kugharamia tafiti ili kupunguza utegemezi wa ufadhili kutoka nje ya nchi na kuwezesha tafiti hizo kuakisi vipaumbele vya kitaifa pamoja na mahitaji ya maendeleo ya taifa. Amesema tafiti zinazofanywa katika chuo hicho kwa kiasi kikubwa zinategemea fedha za ufadhili.

Kwa upande wake, Rasi wa Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Madaktari wa Wanyama Tanzania Prof. Esron Karimuribo, amesema Chama cha Madaktari wa Wanyama Tanzania (TVA) kinaomba marekebisho ya muundo wa utawala katika Serikali za Mitaa kupitia TAMISEMI ili kuwawezesha madaktari wa wanyama kusambaa na kuhudumu katika maeneo mbalimbali nchini, kuanzia ngazi ya Wizara hadi vijijini.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!