Latest Posts

WATOTO WENYE ULEMAVU KUPATA NAFUU YA CHANGAMOTO ZA ELIMU

 

Watoto wenye ulemavu mkoani Geita wanakabiliwa na changamoto ya kupata elimu na kushiriki katika shughuli za kijamii kutokana na ukosefu wa viti mwendo, hali inayowafanya baadhi yao kushindwa kufika shuleni na kuendelea na masomo kama watoto wengine.

Kutokana na changamoto hiyo, Shirika la NELICO Geita, kwa kushirikiana na Chama cha Watu Wenye Ulemavu pamoja na wadau wa habari mkoani humo, limeweka lengo la kukusanya viti mwendo 300 kupitia Marathon ya Watumaini ya Hisani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwasaidia watoto hao, hususan wanaotoka katika familia zenye hali duni za kiuchumi.

Akizungumza wakati wa marathon hiyo iliyofanyika leo mjini Geita, Mkurugenzi wa Shirika la NELICO Geita, Paulina Alex Majogoro, amesema tukio hilo limekuwa la kipekee na lenye mafanikio makubwa, baada ya kufanikiwa kupata ahadi na michango ya zaidi ya viti mwendo 100, huku matumaini yakiwa ni kufikia lengo lililowekwa.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Beyond Inclusion, Flavian Kishekwa, amesema pamoja na lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya ununuzi wa viti mwendo, marathon hiyo pia ilikuwa sehemu ya kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kufanya mazoezi kwa ajili ya kulinda afya na kujenga mshikamano katika kusaidia watu wenye ulemavu.

Nao baadhi ya ndugu na walezi wa watoto walionufaika na msaada wa viti mwendo wameishukuru NELICO pamoja na wadau wengine waliojitokeza kuchangia, wakieleza kuwa vifaa hivyo vitawasaidia watoto wao kupata fursa ya kwenda shule, kushiriki katika shughuli za kijamii na kupunguza changamoto za kuwahudumia katika shughuli za kila siku.

Kupitia marathon hiyo, waandaaji wameeleza kuwa wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na jamii kuhakikisha wanatimiza lengo la kukusanya viti mwendo 300, hatua inayotarajiwa kuwafikia watoto na vijana wengi zaidi wenye ulemavu mkoani Geita na kuwawezesha kupata elimu pamoja na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!