Latest Posts

ASKARI WA TFS NA MIGAMBO WANNE WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUSABABISHA KIFO CHA MTOTO

Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora linawashikilia askari watatu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na askari mgambo wanne kwa tuhuma za kusababisha kifo cha Grace Mussa (4), mwanafunzi wa darasa la awali, na kujeruhi mtu mmoja baada ya kufyatua risasi kwa wananchi waliokuwa wakipinga trekta kukamatwa kwa madai ya kulima ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Taifa wa Kigosi Muyowozi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, SACP Richard Abwao, amesema tukio hilo limetokea Desemba 2, 2024, katika kijiji cha Mpanda Mlowoka, kata ya Igwisi, Wilaya ya Kaliua.

Kamanda Abwao amesema kuwa askari hao walikuwa doria ndani ya hifadhi walipokamata trekta lenye namba za usajili T.689 DCA likiwa limeingia na kulima ndani ya msitu huo. Hata hivyo, wananchi walikusanyika kwa lengo la kuzuia trekta hilo kupelekwa kambini kwa askari hao.

Katika hali ya taharuki, askari hao wakiwa na bunduki mbili aina ya AK-47, walifyatua risasi zilizomsababishia Grace Mussa kifo na kumjeruhi mtu mmoja ambaye kwa sasa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kaliua.

Kamanda Abwao amesema mwili wa marehemu tayari umekabidhiwa kwa familia yake kwa ajili ya mazishi, huku uchunguzi ukiendelea kuhakikisha haki inatendeka. Aidha, askari na migambo waliotuhumiwa wamekamatwa na wanashikiliwa kwa ajili ya taratibu za kisheria.

Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuwa watulivu na kutojihusisha na vitendo vyovyote vya uvunjifu wa sheria, huku likisisitiza umuhimu wa kufuata njia za amani kushughulikia migogoro inayohusu rasilimali za taifa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!