Latest Posts

BOT YATANGAZA NOTI MPYA ZENYE SAINI ZA VIONGOZI WA SASA

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, ametangaza kuwa noti mpya za Tanzania zenye saini ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, na saini yake mwenyewe, zitaanza kutumika rasmi kuanzia tarehe 1 Februari 2025. Noti hizo ni za toleo la mwaka 2010 na zitatumika sambamba na noti zilizopo kwa sasa.

Bw. Tutuba ametoa tangazo hilo wakati akimkabidhi rasmi Waziri wa Fedha, Dkt. Nchemba, sampuli za noti mpya za shilingi 10,000, 5,000, 2,000, na 1,000. Hafla hiyo imefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.

“Mheshimiwa Waziri, nina furaha kukujulisha kuwa zoezi la uchapaji upya wa noti kwa marejeo ya toleo la mwaka 2010 limekamilika, na tumewajulisha wananchi kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye Gazeti la Serikali,” amesema Bw. Tutuba.

Gavana ameeleza kuwa noti hizo mpya zitakuwa na muonekano wa noti zinazotumika sasa, ikiwa ni pamoja na ukubwa, rangi, alama za usalama, na vipengele vingine muhimu. Hata hivyo, mabadiliko yamefanyika kwenye saini.

Saini ya aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dkt. Philip Isdor Mpango, ambaye sasa ni Makamu wa Rais, imebadilishwa na kuwekwa saini ya Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba. Vilevile, saini ya aliyekuwa Gavana wa BoT, Prof. Florens Luoga, imebadilishwa na kuwekwa saini ya Gavana wa sasa, Bw. Emmanuel Tutuba.

Akizungumza baada ya kupokea sampuli za noti hizo, Dkt. Nchemba amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuruhusu mchakato huo kufanyika. Pia amempongeza Gavana wa BoT kwa kusimamia uchapaji wa noti hizo kwa uadilifu na weledi mkubwa.

“Hii ni hatua kubwa kwa taifa letu na inaendeleza heshima kwa wataalamu wetu wa ndani kwa kusimamia kwa umakini mambo yenye maslahi mapana kwa nchi yetu,” amesema Dkt. Nchemba.

 

Waziri Nchemba ameridhia noti hizo kuanza kutumika rasmi kama ilivyopangwa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!