Latest Posts

DAWA ZA BILIONI 12 ZILIHIFADHIWA HADI KUISHA MUDA WAKE- CAG

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imebaini uzembe na ucheleweshaji wa maamuzi katika taasisi mbalimbali za umma, hali iliyosababisha mali za serikali zenye thamani ya mabilioni ya shilingi kutotumika kwa muda mrefu, huku nyingine zikiendelea kuharibika.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, magari 552, pikipiki 98 na mashine 20 hazijatumika kwa muda mrefu katika taasisi 81, bila hatua yoyote ya matengenezo wala kuuzwa, kutokana na ucheleweshaji wa maamuzi na ukosefu wa mipango madhubuti ya matumizi. Aidha, ripoti imebaini majengo na mitambo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 37.07 hayatumiki, yakiwemo jengo la Shirika la IPS lililodumu miaka mitatu bila kutumika, mitambo ya Bohari ya Dawa tangu mwaka wa fedha 2020/2021, na baadhi ya majengo ya utalii katika hifadhi za Taifa.

“Hali hii imesababishwa na ukosefu wa fedha za ukarabati, ucheleweshaji wa manunuzi, na ukosefu wa mpango wa matumizi, hivyo kusababisha hasara na kuathiri huduma kwa wananchi,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Katika sekta ya afya, ukaguzi umebaini dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 12.44 vimeharibika kutokana na kuisha muda wa matumizi bila kuondolewa. Ripoti inaeleza kuwa sababu kuu za hali hiyo ni pamoja na ucheleweshaji wa vibali vya kisheria vya kuondoa dawa hizo, ununuzi usiozingatia tathmini ya mahitaji halisi, na kutofuata utaratibu wa FIFO (First In, First Out).

Mbali na hilo, ripoti imebaini kuwa taasisi 269 za umma zinadaiwa jumla ya Shilingi Bilioni 311.98 kwa ajili ya madeni ya watumishi. Kati ya deni hilo, Serikali Kuu inadaiwa Shilingi Bilioni 274.8 (sawa na asilimia 88), Mamlaka za Serikali za Mitaa Shilingi Bilioni 24.54 (asilimia 8), na Mashirika ya Umma Shilingi Bilioni 12.64 (asilimia 4). Madeni hayo yanahusisha mishahara, gharama za usafiri kwa wastaafu na marupurupu mbalimbali.

CAG ameeleza kuwa chanzo kikuu cha madeni haya ni ufinyu wa bajeti, ucheleweshaji wa fedha, pamoja na udhaifu wa usimamizi wa fedha za umma.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!