Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewazawadia wahitimu wawili bora wa Chuo cha Maji, Florence Theonist na Emmanuel Nyaki, kompyuta mpakato na fedha taslimu shilingi milioni sita (milioni 3 kwa kila mmoja) kama sehemu ya kutambua juhudi zao katika masomo na kuwahamasisha vijana wengine kujiunga na kozi za zinahusu masuala ya maji.
Akikabidhi zawadi hizo Waziri wa Maji, Jumaa Aweso katika mahafali ya 48 ya Chuo cha Maji yaliyofanyika Novemba 13, 2024, jijini Dar es Salaam amesema motisha kama hizi huleta chachu na bidii kwa wanafunzi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa EWURA baada ya hafla hiyo, David Linda, Mhandisi Mwandamizi wa Maji na Usafi wa Mazingira amebainisha kuwa lengo la zawadi hizo ni kuhamasisha vijana wengi kujiunga na kozi za sekta ya maji ili kuwa na wataalamu wengi watakaosaidia katika kutoa huduma bora na kuchangia maendeleo ya sekta hiyo.
“EWURA, kama mdhibiti wa sekta ya maji, inatambua umuhimu wa kuwa na wataalamu wa kutosha ili kutoa huduma bora, moja ya Malengo Endelevu ya Dunia (SDGs) ni kuwezesha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wote, hii halitowezekana kama hatutakuwa na wataalamu wa kutosha ndio maana EWURA iko mstari wa mbele kushirikiana na Chuo cha Maji ili kuandaa wataalamu wenye uwezo wa kufanikisha lengo hili,” amesema Linda.
Florence Theonest, mmoja wa wahitimu waliotunukiwa, ameishukuru EWURA kwa zawadi hiyo na kueleza kuwa kompyuta aliyopokea itamsaidia katika kazi za kiufundi, hasa ikizingatiwa kuwa shughuli nyingi za uhandisi wa maji zinategemea programu mbalimbali za kiteknolojia.