Aliyekuwa Naibu wa Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, ametoa kauli nzito akidai kuwa viongozi wa nchi za Afrika Mashariki wameanza kuambukizana “tabia mbaya” ya kutumia mabavu kunyamazisha wakosoaji na viongozi wa upinzani.
Akizungumza katika mahojiano maalum na BBC, Gachagua amebainisha kuwa mazingira ya kisiasa nchini Kenya yameanza kufanana na yale ya nchi jirani, ambapo viongozi wa upinzani kama Tundu Lissu (Tanzania) na Kizza Besigye (Uganda) wanashikiliwa gerezani.
Gachagua amekosoa kile alichokiita mwendo wa viongozi wa kanda hiyo kugeukiana na kuanza kuwanyamazisha watu wanaojaribu kuwakosoa. Alipoulizwa kwanini hali hiyo inashamiri sasa, alikuwa na majibu ya moja kwa moja: “Hao viongozi wa Afrika Mashariki wameambukizana tabia mbaya. Kenya ni tofauti sana na Uganda. Kenya ni tofauti sana na Tanzania. Wakenya ni watu ambao hawawezi kubali kutawaliwa na mabavu. Hawawezi kukubali mauaji”.
Gachagua, ambaye aliondolewa madarakani kwa mchakato wa kushitakiwa miezi kadhaa iliyopita, ameeleza kuwa amekuwa akiishi kwa hofu kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara kwenye mikutano yake. Amedai kuwa tangu afurushwe ofisini, amekumbana na vurugu mara 24, zikiwemo zile zinazofanyika ndani ya nyumba za ibada.
“saa ingine naogopa sana juu ya maisha yangu na watu wangu, familia yangu na wafuasi wangu kwa sababu tangu nifurushwe ofisini nimeletewa vita kanisani na nje ya kanisa mara 24. Nimeripoti kwa polisi hakuna hatua yoyote imechukuliwa, na mimi nikiogopa hawa watakuwa wamefaulu. Kwahivyo, mimi nikihisi baridi niogope nirudi nyumbani hapa Wamunyoro ama Nairobi nikae hawa watu watakuwa wamefaulu, kwahivyo mimi naendelea”, amesema.
Kuhusu mustakabali wake wa kisiasa, Gachagua amethibitisha kuwa atagombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Amesema yuko katika mazungumzo na viongozi wengine sita au saba wa upinzani (akiwemo Kalonzo Musyoka na Fred Matiang’i) ili kuunda muungano mmoja utakaomng’oa Rais William Ruto.
Gachagua ambaye pia ni kiongozi mkuu wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) amejitetea dhidi ya madai kuwa yeye ni kiongozi wa ukabila anayejali maslahi ya Mlima Kenya pekee, akisema kuwa siasa zote zinaanzia nyumbani. Amesema kuwa huwezi kutafuta umaarufu kwa jirani ikiwa nyumbani kwako hukubaliki, hivyo kuanza na watu wa Mlimani ni mkakati wa kujiimarisha kitaifa.