Helikopta ya kijeshi ya Uganda iliyokuwa imepelekwa nchini Somalia kama sehemu ya Kikosi cha Amani cha Umoja wa Afrika (AUSSOM) imeanguka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mogadishu Jumatano, na kusababisha vifo vya watu watano, kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la Uganda, Felix Kulayigye.
Amesema kuwa kati ya watu wanane waliokuwemo ndani ya helikopta hiyo, watatu walinusurika lakini walipata majeraha makubwa na kuungua vibaya.
Mlipuko baada ya kuanguka kwa helikopta hiyo ulisababisha milipuko ya silaha zilizokuwa ndani ya helikopta, na kuliharibu majengo ya karibu na kujeruhi raia watatu,” alisema Kulayigye.
Taarifa kutoka kwa ujumbe wa AUSSOM imeeleza kuwa operesheni ya uokoaji bado inaendelea, na juhudi zinafanyika kuwaokoa wahanga waliokuwa ndani ya helikopta hiyo kabla ya kutua.
Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali ya Somalia, SONNA, helikopta hiyo iliwaka moto muda mfupi baada ya kuanguka. “Tuliona moshi mkubwa ukifunika kabisa helikopta, na tulisikia mlipuko mkubwa,” alisema Farah Abdulle, mfanyakazi wa uwanja wa ndege.
AUSSOM, ambayo ni sehemu ya jitihada za kimataifa kuisaidia serikali ya Somalia kupambana na kundi la wanamgambo wa al Shabaab, ina zaidi ya askari 11,000 wanaosaidia katika shughuli za ulinzi na ustawi nchini humo.
Kundi la al Shabaab linaloshirikiana na mtandao wa kigaidi wa al Qaeda limekuwa likipambana na serikali ya Somalia kwa zaidi ya miongo miwili, likijaribu kuangusha serikali inayotambuliwa kimataifa na kuanzisha utawala wake unaotafsiriwa kwa misingi mikali ya sheria za Kiislamu (Sharia).