Hali ya usalama imezidi kuwa tete duniani baada ya Serikali ya Iran kuthibitisha kuuawa kwa mkuu wake wa usalama, Ali Larijani, na kamanda wa kikosi cha Basij, Gholamreza Soleimani, katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Israel.
Mauaji haya yanatajwa na Israel kama pigo kubwa zaidi kwa Iran tangu kuanza kwa mgogoro huo Februari 28, 2026, uliogharimu maisha ya Kiongozi Mkuu Ayatollah Khamenei.
Baraza Kuu la Usalama la Taifa la Iran limethibitisha kuwa Larijani ameuawa akiwa pamoja na mwanawe, msaidizi wake, na Naibu Mkuu wa Usalama, Alireza Bayat. Kupitia shirika la habari la Mehr, baraza hilo limemtaja Larijani kama “shahidi” aliyefikia kilele cha ndoto yake ya kuitumikia Mapinduzi ya Kiislamu.
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, amesema operesheni hiyo ni sehemu ya kampeni endelevu ya kuangamiza uongozi wa Iran na kuudhoofisha utawala huo. Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, katika video aliyoituma leo, amemwita Larijani “bosi wa genge la wahalifu,” akisisitiza kuwa lengo la Israel ni kuwapa Wairani fursa ya kuupindua utawala uliopo.
“Huu ni mkakati wetu wa mwisho wa kuleta mabadiliko ya utawala nchini Iran (Regime Change),” ilieleza taarifa ya jeshi la Israel, ikidai kuwa mauaji ya Soleimani pia ni adhabu kwa kitendo chake cha kukandamiza waandamanaji mwezi Januari nchini humo.
Mkuu wa Jeshi la Iran, Amir Hatami, ametishia kutoa jibu “la majuto” kwa Marekani na Israel kwa wakati na mahali mwafaka. Hata hivyo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran (IRGC) limeonekana kutosubiri, ambapo shirika la habari la AFP limeripoti kuwa IRGC tayari imerusha mfululizo wa makombora katikati mwa Israel kama hatua ya awali ya kulipiza kisasi cha damu ya Larijani.