Latest Posts

KAULI ZA CHALAMILA ZALAUMIWA KUHAMASISHA RUSHWA KWENYE AFYA

Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA) taifa limeeleza masikitiko yake makubwa juu ya kauli iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, aliyesema kuwa, “Wajawazito wasiotaka kununua glavu wakajifungulie nyumbani.”

Kauli hiyo iliyotolewa wakati wa mkutano na wananchi wa Temeke imeelezwa kuwa ya udhalilishaji, isiyo na staha, na inayokinzana na haki za afya ya mama na mtoto.

Kwa mujibu wa taarifa ya BAWACHA iliyotolewa siku ya Jumanne Januari 28, 2025 na Sigrada Wilhem Mligo, Mratibu wa Uenezi BAWACHA Taifa, kauli ya Chalamila inaenda kinyume na Sera ya Afya ya Taifa na Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya (HSSP-V) wa mwaka 2021-2026 unaolenga kuboresha huduma za afya ya uzazi.

“Kujifungulia nyumbani ni hatari kwa afya ya mama na mtoto, kwani kunaongeza uwezekano wa maambukizi ya vimelea vya magonjwa (sepsis) na kukosa huduma ya dharura endapo matatizo yatatokea”, imesisitiza BAWACHA.

Baraza hilo limeeleza wasiwasi kwamba kauli ya Chalamila inaweza kufungua mianya ya rushwa kwa watoa huduma wasiokuwa waaminifu, ambao wanaweza kuwataka wajawazito kulipia huduma ambazo zinapaswa kuwa bure.

BAWACHA imesema, “Kauli hii inahamasisha vitendo vya rushwa na inaweza kuchochea ukosefu wa uwajibikaji miongoni mwa watoa huduma za afya.”

BAWACHA pia imetaka Wizara ya Afya kutoa ufafanuzi wa wazi juu ya huduma za afya ya mama na mtoto. Baraza hilo limesema kwamba kuna mkanganyiko mkubwa kuhusu iwapo huduma hizi ni bure kama inavyodaiwa na sera, au kama zinahitaji gharama ambazo wananchi hawajui waziwazi.

Katika taarifa yake, BAWACHA imetoa wito kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kuchukua hatua dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kauli hiyo, ikisema, “Ni muhimu viongozi wa umma wawe na staha wanapozungumza na wananchi, hasa wanaposhughulikia masuala nyeti kama afya ya mama na mtoto.”

Baraza hilo limewasihi watoa huduma wa sekta ya afya kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia maadili yao ya taaluma na utu, bila kujali changamoto zinazotokana na kauli au matendo ya baadhi ya wanasiasa.

BAWACHA imeonya kwamba, iwapo hatua hazitachukuliwa dhidi ya RC Chalamila, watatoa wito kwa wananchi kumkataa.

“Hatuwezi kukaa kimya wakati viongozi wa umma wanatoa kauli zinazochochea maumivu kwa wanawake wa kawaida ambao wanakosa uwezo wa kumudu gharama za afya,” wamesisitiza.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!