Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, amepata ushindi mwingine wa karibu asilimia 100 katika uchaguzi wa Bunge la nchi hiyo (Supreme People’s Assembly), huku kukiwa na mabadiliko ya nadra katika ripoti za matokeo yaliyotangazwa na vyombo vya habari vya serikali.
Katika uchaguzi uliofanyika Machi 15, 2026, chama tawala cha Workers’ Party of Korea na washirika wake wameshinda kila kiti kati ya viti 687 vya bunge hilo. Hata hivyo, tofauti na miaka ya nyuma ambapo ushindi ulikuwa asilimia 100, safari hii serikali imekiri kuwepo kwa asilimia 0.07 ya wapiga kura walioikataa serikali.
Nchini Korea Kaskazini, hakuna wagombea wa upinzani. Katika kila jimbo, wapiga kura hupewa mgombea mmoja aliyepitishwa na serikali na wana hiari ya kumkubali au kumkataa.
Asilimia hiyo 0.07 haikuenda kwa mpinzani, bali inawakilisha kundi dogo la raia walioamua kupiga kura ya “hapana” dhidi ya wagombea rasmi. Hii ni mara ya kwanza kwa utawala wa Kim kukiri hadharani kuwepo kwa kura za kupinga tangu miaka ya 1950.
Shirika la habari la KCNA limeripoti kuwa mahudhurio ya wapiga kura yalikuwa ni asilimia 99.99, ambao hawakupira kura ni asilimia 0.0037 tu (walio nje ya nchi au kazini baharini). Asilimia 0.00003 pekee ndio waliochagua kutopiga kura kabisa.
Tangu aingie madarakani mwaka 2011, Kim Jong Un amezidi kuimarisha mamlaka yake. Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2019 yalimfanya kuwa Mkuu wa Nchi mwenye mamlaka kamili na “yasiyotikisika” juu ya jeshi, serikali, na taasisi zote za nchi.