Hatua za kimkakati za kutangaza vivutio vya utalii nchini Tanzania zilizochukuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, zinaendelea kuzaa matunda, huku Hifadhi ya Urithi wa Utamaduni wa Dunia ya Magofu ya Kale ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara ikishuhudia ongezeko kubwa la watalii kutoka mataifa mbalimbali
Hifadhi hiyo, inayosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), imeanza mwaka 2025 kwa mafanikio makubwa. Mnamo Januari 18, 2025, iliwapokea watalii 98 wa kimataifa, na Januari 22, 2025, iliwapokea watalii wengine 173 kutoka Uingereza, Finland, Seychelles, Marekani, Sweden, Australia, na Ireland.
Watalii hao walifika kwa meli kubwa aina ya Hebridean Sky, kwa lengo la kufurahia vivutio vya kihistoria vilivyopo kwenye hifadhi hiyo.
Hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kushiriki filamu ya Royal Tour, iliyolenga kufufua sekta ya utalii baada ya athari za janga la UVIKO-19, imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza wageni wa kimataifa. Filamu hiyo imeweka Tanzania katika ramani ya utalii duniani, na kuhuisha shughuli za kitalii ambazo zilisitishwa au kupungua kwa sababu ya mdororo wa uchumi wa dunia.
Mafanikio haya yameifanya TAWA kuwa moja ya taasisi za kiuhifadhi zilizonufaika zaidi. Idadi ya watalii wanaotembelea maeneo yake kwa utalii wa picha na uwindaji wa kitalii imeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Kwa mujibu wa taarifa, katika kipindi cha mwaka 2023/24, Hifadhi ya Urithi wa Utamaduni wa Dunia ya Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara ilipokea meli 9 za kitalii na jumla ya watalii 1,047 wa kimataifa.
Ongezeko hili linaonesha jinsi juhudi za serikali na viongozi wake zimeendelea kuimarisha sekta ya utalii nchini.