Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimekemea vikali kauli ilizozitaja kuwa za udhalilishaji na zinazotweza utu wa mwanamke zinazodaiwa kutolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, wakati wa hafla ya hadhara iliyofanyika wilayani Temeke, Dar es Salaam.
Katika hafla hiyo, iliripotiwa kuwa Chalamila alimjibu mama aliyelalamikia huduma duni hospitalini kwa maneno ya kejeli, akisema,
“Toka nje chukua bajaji, nenda zako nyumbani kamwambie mumeo achukue visu na mikasi akusaidie kujifungua.”
Kauli hii imeelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dkt. Anna Henga alipokuwa akizungumza na wanahabari siku ya Jumanne tarehe 28, 2024 mkoani Dar es Salaam, kuwa si tu inatweza utu wa mwanamke, bali pia inakiuka misingi ya maadili, haki za binadamu, na utawala bora.
Kwa mujibu wa LHRC, afya ya uzazi ni haki ya msingi inayolindwa na ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Pia, sera ya afya ya mwaka 2007 inatamka wazi kuwa huduma za msingi za afya, ikiwa ni pamoja na huduma za mama na mtoto, zinapaswa kutolewa bure katika vituo vya afya vya serikali.
Hata hivyo, LHRC imebainisha kuwa changamoto za utekelezaji wa sera hiyo bado ni tatizo nchini, ikiwemo ukosefu wa vifaa vya msingi kama mikasi, glovu, na dawa muhimu. Changamoto hizi mara kwa mara zinasababisha wanawake kulazimika kulipia huduma zinazotakiwa kutolewa bure.
Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2023 ilionesha kuwa vifo vya kina mama wajawazito nchini mara nyingi hutokana na uzembe wa watumishi wa afya, kuchelewa kwa huduma, au ukosefu wa vifaa muhimu hospitalini. Katika baadhi ya matukio, kauli za kejeli kutoka kwa watumishi wa afya zimehusishwa na madhila wanayokumbana nayo wajawazito.
Kwa mfano, mwaka 2024, mama mjamzito katika Wilaya ya Muheza, Mkoa wa Tanga, alifariki dunia kutokana na uzembe wa watumishi wa kituo cha afya. LHRC inasema kuwa matukio kama haya yanapaswa kutokomezwa kwa kuchukua hatua madhubuti za uwajibikaji.
LHRC imetoa wito kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya Albert Chalamila kwa kauli zake zilizotajwa kuwa za udhalilishaji. Pia, LHRC imeitaka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kumhoji Chalamila iwapo hatua za kinidhamu hazitachukuliwa.
Aidha, LHRC imehimiza maboresho katika mitaala ya mafunzo kwa kada ya afya, hususan kuhusu matumizi ya lugha yenye staha na kujali katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
LHRC imekumbusha kuwa viongozi wa umma wanawajibika kwa wananchi kama ilivyoainishwa katika ibara ya 8 ya Katiba ya Tanzania, na kwamba kauli za kejeli na udhalilishaji zinapunguza imani ya wananchi kwa serikali na zinakwamisha juhudi za kukuza utawala wa sheria na haki za binadamu nchini.