Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini (LHRC) kimetoa wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini sambamba na mamlaka za kisheria kuhakikisha vinafuata sheria pindi vinapomkamata mtu/ watu ikiwemo kuwafikisha Mahakamani ndani ya muda unaokubalika kisheria
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Jumatatu Oktoba 21.2024, Mkurugenzi mtendaji wa LHRC Dkt. Anna Henga amesema wakati huu (leo) ambao Afrika inaadhimisha siku ya Haki za Binadamu, Tanzania imekuwa na matukio yenye viashiria vya uvunjifu wa Haki za Binadamu kwa namna moja au nyingine
Amesema siku za hivi karibuni kupitia taarifa mbalimbali kutoka kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kumeshuhudiwa taarifa za uwepo wa matukio ambayo amedai kuwa yanaonekana kukiuka misingi ya ‘Haki za Binadamu na Utawala Bora, ambapo katika hilo ametolea mfano taarifa iliyosambaa nchini Oktoba 20.2024 inayomuhusisha Katibu Mwenezi wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA) Aisha Machano anayedaiwa kutekwa, kupigwa kisha kutupwa porini
“Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa yeye mwenyewe Bi Aisha alibainisha kuwa mnamo tarehe 19 Oktoba 2024 akiwa katika kituo cha daladala wilayani Kibiti alivamiwa na wanaume sita na mwanamke mmoja waliojitambulisha kuwa ni maafisa wa Jeshi la Polisi na kisha kumkamata, taarifa hiyo inadai kuwa Bi Aisha aliteswa na kufhalilishwa kijinsia na hatimaye kupoteza fahamu kisha kumtelekeza maporini” -Dkt. Henga
“Baada ya fahamu kumrejea alijikuta akiwa katika Hospitali ya rufaa ya Mwananyamala huku akiwa na majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake, taarifa hiyo ilithibitishwa na Jeshi la Polisi makao makuu ambapo Jeshi hilo lilibainisha kuwa linafanya uchunguzi juu ya tukio hilo” -Dkt. Henga
Aidha, LHRC imelaani vikali vitendo vya kukamatwa na kuumizwa kwa Watanzania wasiokuwa na hatia, haswa ikizingatiwa kuwa muathirika wa tukio tajwa ni mwanamke
Kituo hicho kimeendelea kusisitiza kuwa vitendo vya kunyanyasa na kuumiza wanawake hususani wanaojihusisha na siasa katika kipindi hiki cha uchaguzi havikubaliki kwani ni kinyume na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania ni mwanachama wake
Pia, LHRC imetoa wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini kuwasaka, kuwatia mbaroni na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watendaji wa matukio ya aina hiyo ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao
“Aidha kwa nyakati tofauti kumekuwa na ripoti za kukamatwa kinyume cha sheria kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa huku taarifa hizo zikithibitishwa na Makamanda wa Polisi wa mikoa ambayo matukio hayo yametendeka pamoja na baadhi ya taarifa kutolewa na makao makuu ya Jeshi la Polisi
LHRC imerejea tukio la kukamatwa kwa Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Katavi Rhoda Kunchela lililotokea Oktoba 18.2024, sambamba na tukio la kukamatwa kwa Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Iringa mjini Frank Nyalusi, tukio ambalo baadaye Jeshi la Polisi lilitoa taarifa za kuachiliwa kwa kiongozi huyo kwa dhamana.