Latest Posts

MASWI AITAKA WIZARA YA KATIBA NA TLS KUSHIRIKIANA KWA MASLAHI YA TAIFA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Eliakim Maswi, ametoa wito kwa Wizara hiyo na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kushirikiana kwa manufaa ya Taifa katika mapambano dhidi ya utakatishaji wa fedha haramu.

Akizungumza katika kikao kazi kilichofanyika tarehe 31 Oktoba, 2024, jijini Dodoma, Bw. Maswi amesema kuwa kujenga Taifa imara kunahitaji ushirikiano wa dhati kati ya taasisi mbalimbali ili kuhakikisha sheria ya udhibiti wa fedha haramu inatekelezwa ipasavyo.

Maswi amesisitiza kuwa kuna watu wasio waadilifu ambao wanaweza kushiriki katika vitendo vya utakatishaji fedha, jambo ambalo linakiuka sheria na kuhatarisha usalama wa Taifa. Ameitaka TLS na wadau wengine kuendelea kujengeana uwezo na kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu ya kisheria kwa lengo la kudhibiti vitendo vya fedha haramu.

Naye Kamishna wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU), Bi. Fatma Simba, ameongeza kuwa utakatishaji fedha haramu unaleta madhara makubwa ya kiuchumi, kijamii, kisiasa, na kiusalama, na unahatarisha utawala wa sheria. Amesema jitihada za pamoja zinahitajika ili kukabiliana na biashara hiyo haramu.

Kwa upande wake, Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi, ameeleza kuwa TLS inasimamia Katiba na sheria za nchi na iko tayari kushirikiana na Wizara katika masuala yote yanayolenga kuimarisha maslahi ya Taifa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!