Latest Posts

MBEYA DC YATUMIA ZAIDI YA BILIONI 150 KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO

Na Josea Sinkala, Mbeya.

 

Halmashauri ya wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya imepokea na kutumia fedha zaidi ya shilingi billion 150 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kwa mujibu wa afisa mipango katika Halmashauri ya wilaya ya Mbeya Ozana Omary, akitoa maelezo kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo, fedha hizo zimetolewa kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Disemba 2024 kwa ajili ya utekelezwaji wa miradi mbalimbali ikiwemo kujengwa kwa shule mpya za sekondari Ihombe na Lwanjilo, sekta ya afya na kwingineko.

Bi. Ozana amesema pia katika fedha hizo pia kuna fedha zitokanazo na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Mbeya na kwamba mabillion hayo ya fedha yaligawiwa kwa taasisi mbalimbali za kiserikali wakiwemo RUWASA na TANESCO katika kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo.

Baada ya uwasilishaji taarifa hiyo, mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Mbeya vijijini Akimu Mwalupindi, amewapongeza madiwani, wataalam na viongozi wengine wa chama hicho katika kata na vijiji vyao kwa ushirikiano na kamati ya siasa Wilaya kuhakikisha miradi mbalimbali inaendelea kama ilivyo dhamira ya Serikali.

Mwalupindi amewataka viongozi hao kuendelea kushirikiana ikiwemo kuendelea kusemea miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa ili jamii ijue hasa wakati huu wa kwenda kupimwa kwa viongozi mbalimbali kuelekea uchaguzi mkuu.

Amesema kwenye uchaguzi huo kila mmoja atapimwa kwa kazi yake au atakavyowapambania wananchi na kwamba hakuna mwenye nafasi bali ni haki ya kila mtu hasa wakati utakapofika wa kutia nia na kugombea badala ya kuanza kujipitisha mapema kwenye kata na majimbo mbalimbali.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!