Mradi wa kiwanda cha kuzalisha mafuta ya kupikia ya alizeti, unaojengwa katika Kijiji cha Veyula, Dodoma, umeonesha maendeleo chanya tangu uliposajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) mwaka 2023. Mradi huu, wenye mtaji wa dola za Kimarekani milioni 60, unatarajiwa kuanza rasmi uzalishaji mwaka huu kwani hadi sasa, ujenzi na ufungaji wa vifaa vimefikia asilimia 90.
Kukamilika kwa mradi huu kutatoa ajira kwa watu 500, hatua inayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Dodoma na maeneo ya jirani.
TIC imeonesha umuhimu wa huduma zake za mahala pamoja kwa kuhakikisha wawekezaji wanapata msaada wa haraka kusajili miradi yao na kuanza utekelezaji kwa wakati. Hii inasaidia sana kupunguza ucheleweshaji wa miradi ya maendeleo na kuvutia uwekezaji zaidi nchini Tanzania.
Kupitia juhudi hizi, Dodoma inazidi kuwa kitovu cha uwekezaji, ikithibitisha kuwa mazingira rafiki ya uwekezaji yanaweza kuleta matokeo ya haraka na yenye tija.