Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Tawi la Machinjioni, Kata ya Makongorosi Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya, Michael Kalinga ameelezwa kukutwa akiwa ameuawa, na mwili wake kutelekezwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na tovuti ya Mwananchi, tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia siku ya Jumanne, Desemba 3, 2024, na mwili wake kukutwa kata ya Mkola, huku Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Wilbert Siwa akisema kuwa wamepata taarifa za mauaji ya Kalinga na wanaendelea kuzifanyia kazi.
Katibu wa CCM Wilaya Chunga, Charles Jockel akizungumza na tovuti hiyo amesema bado haijulikani ikiwa Michael Kalinga alikuwa anakwenda au kurudi Makongorosi kwa kuwa mwili wake ulikutwa eneo la kuelekea Kata ya Mkola, akiongeza kuwa kwa sasa wanaviachia vyombo vya dola kufanya uchunguzi kuhusu tukio hilo.
Kwa upande wake Mbunge wa Lupa (CCM), Masache Kasaka amedai katika Mamlaka ya Mji wa Makongorosi matukio ya watu kuuawa yamekuwa yakijirudia mara kwa mara licha ya kuwepo kwa kituo kikubwa cha polisi, jambo ambalo amelitaja kujenga hofu kwa wananchi kufanya shughuli za kiuchumi na kupunguza nguvu kazi kwa Taifa.