Na Shabih Kassim.
Shirika la habari la The Guardian limeripoti kuwa ndege ya abiria ya Angara Airlines imeanguka katika eneo la mashariki ya mbali mwa Urusi baada ya kutoweka kwenye rada na kupoteza mawasiliano na waelekezaji wa ndege wakati ikikaribia kutua katika mji wa Tynda, mkoa wa Amur, karibu na mpaka wa China.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tass, uchunguzi wa anga ulibaini kutokuwepo kwa manusura. “Kwa taarifa za awali, hakuna aliyeokoka. Hadi sasa helikopta ya uokoaji haijafanikiwa kutua eneo la ajali,” alisema afisa mmoja wa dharura.
Mabaki ya ndege aina ya An-24 yalipatikana yakiwa yanawaka moto umbali wa takribani kilomita 14 kutoka uwanja wa ndege wa Tynda. Vyombo vya habari vya Urusi vimeonesha moshi mzito ukitanda juu ya msitu mnene.
Gavana wa Amur, Vasily Orlov, alisema kulikuwa na abiria 43, wakiwemo watoto watano, na wafanyakazi sita ndani ya ndege. Kamati ya uchunguzi ya usafiri nchini Urusi imesema kuwa hitilafu ya kiufundi au kosa la kibinadamu vinachunguzwa kama chanzo cha ajali hiyo.
Ndege hiyo ya An-24, iliyojengwa mwaka 1976, inatambulika kwa uimara wake na uwezo wa kuruka kwenye viwanja visivyo na lami, hasa katika maeneo ya mbali ya Urusi. Hii ni ajali ya kwanza ya vifo kwa ndege ya abiria nchini humo tangu mwaka 2021. Tangu kuanza kwa vita vya Ukraine, sekta ya anga ya Urusi imeathirika vibaya kutokana na vikwazo vya Magharibi vilivyosababisha uhaba wa vipuri na kukamatwa kwa ndege nyingi za kigeni.
Kwa mujibu wa The Guardian, mashirika ya ndege kadhaa yaliomba kuongeza muda wa matumizi ya ndege za An-24 mwaka 2023 kutokana na ukosefu wa mbadala. Ripoti ya Agentstvo imebainisha kuwa ndege hiyo ya Angara ilishawahi kukumbwa na matatizo ya kiufundi mwaka 2022 na mapema mwaka huu.