Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gelard Kusaya, amekabidhi msaada wa zawadi mbalimbali zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa wazee wanaoishi katika Kituo cha Kulelea Wazee cha Nyabange kilichopo wilayani Butiama. Zawadi hizo ni pamoja na mbuzi, mchele, unga, mafuta ya kupikia, sukari, na vinywaji.
Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo, Kusaya alisema kuwa hatua hiyo ni ishara ya upendo na kuthamini mchango wa wazee hao katika jamii. Alisisitiza kuwa serikali inaendelea kuwajali wazee kwa vitendo, huku akiwasihi waendelee kumuombea maisha marefu Rais Dkt. Samia.
“Endeleeni kumuombea na kumwamini Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu. Hakika ni kiongozi anayejali watu wake na hataki kuona wakiteseka. Zawadi hizi ni sehemu ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa, hivyo tunasherehekea pamoja nanyi. Kamwe hamtasahaulika,” alisema Kusaya.
Kwa niaba ya wazee, George Ndege alitoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia kwa msaada huo. Hata hivyo, alieleza changamoto ya uchakavu wa majengo ya kituo hicho na kuiomba serikali kuyakarabati ili kuboresha mazingira ya kuishi.