Serikali ya Tanzania imefanya tathmini ya awali ya mradi wa Treni ya Mwendokasi ya SGR na kubaini kuwa mradi huo umetoa manufaa makubwa kiuchumi na kijamii.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema kuwa mradi huu umeshazalisha ajira zaidi ya 30,176 za moja kwa moja na ajira 150,000 zisizo za moja kwa moja, na umeingiza pato la shilingi bilioni 358.74.
Prof. Mkumbo ametoa taarifa hiyo tarehe 1 Novemba, 2024, wakati akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2025/2026 bungeni jijini Dodoma.
Waziri Prof. Kitila ameeleza kuwa mradi umetoa fursa kwa viwanda na wakandarasi, na hadi sasa kampuni 2,460 zinashiriki katika mradi huo, huku kandarasi za thamani ya shilingi trilioni 3.69 zikiwa zimetolewa.
Aidha, mradi umeongeza mahitaji ya saruji, nondo, na vifaa vingine vya ujenzi, hivyo kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda na kupunguza muda wa safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma kutoka wastani wa masaa kumi kwa basi hadi masaa matatu na nusu kwa treni.
“Mradi umechochea kuongezeka kwa mahitaji ya saruji, nondo, na vifaa vingine vya ujenzi na kuongeza mchango wa sekta ya viwanda katika Uchumi”, amesema Prof. Kitila.
Prof. Mkumbo amebainisha faida nyingine za mradi, ikiwemo kupunguza ajali na kuokoa maisha ya watu, kutunza mazingira kwa kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa, na kuongeza kipato ambapo hadi Septemba 2024, abiria 645,421 wamesafirishwa na kiasi cha shilingi bilioni 15.695 kimepatikana. Pia, mradi umechochea utalii kwenye hifadhi za Mikumi, Ruaha, Katavi, Gombe, na Serengeti kupitia vituo vilivyo katika ukanda wa reli.
Mradi huo unatarajiwa kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo na abiria, hivyo kuchochea ukuaji wa biashara za ndani na kimataifa. Prof. Mkumbo amefichua kuwa hadi Septemba 2024, miradi 519 yenye thamani ya dola bilioni 4.59 za Kimarekani na ajira 115,566 imesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji (TIC) kwenye ushoroba wa reli, ambapo baadhi ya miradi hiyo imekamilika na imeanza uzalishaji.
Hadi sasa, Serikali imewekeza dola bilioni 10 za Kimarekani (sawa na shilingi trilioni 23) kwenye mradi wa SGR tangu ujenzi ulipoanza Mei 2, 2017, na kipande cha reli kati ya Dar es Salaam na Dodoma kimeshakamilika na kimeanza kazi.