Latest Posts

TANZANIA HUENDA IKAZUIA BIDHAA ZA KILIMO ZA MALAWI, AFRIKA KUSINI

Serikali ya Tanzania imeipa Malawi na Afrika Kusini muda wa hadi Jumatano ijayo kufungua masoko yao kwa mazao ya kilimo kutoka Tanzania, la sivyo itachukua hatua ya kuzuia bidhaa zote za kilimo kutoka nchi hizo kuingia nchini pamoja na kupita katika ardhi ya Tanzania kuelekea kwenye masoko mengine.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ametangaza hatua hiyo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, asubuhi ya Alhamisi Aprili 17, 2025, ambapo amesema kuwa Tanzania imechoshwa na vikwazo visivyo na maelezo vinavyowekwa na baadhi ya nchi jirani dhidi ya mazao ya Watanzania.

“Tupokee taarifa kuwa nchi ya Malawi imezuia mazao mbalimbali kuingia nchini kwao. Mazao hayo ni pamoja na unga, mchele, tangawizi, ndizi na hata mahindi, jambo ambalo limesababisha wafanyabiashara wetu wa Kitanzania kushindwa kuingiza mizigo katika nchi hiyo,” amesema Bashe.

Amesema kuwa kwa miaka mitano, Tanzania imekuwa ikijitahidi kufungua soko la Afrika Kusini kwa zao la ndizi bila mafanikio, hali inayofanana na jitihada za miaka 10 zilizochukua muda mrefu kufanikisha uuzaji wa parachichi nje ya nchi hiyo.

“Kwa mara ya mwisho, tunaendelea na jitihada za mawasiliano na Serikali za ‘South Africa’ na Malawi hadi kufikia Jumatano ijayo. Tukikosa mrejesho, Wizara ya Kilimo itazuia mazao yote ya kilimo na bidhaa zote kutoka South Africa na Malawi,” amesisitiza.

Aidha, amesema kuwa Tanzania haitaruhusu tena mazao kutoka Malawi au Afrika Kusini kutumia ardhi ya Tanzania kwenda katika bandari ya Dar es Salaam au nchi nyingine, na kwamba hatua kama hiyo iliwahi kuchukuliwa mwaka jana hadi mataifa hayo yalipofungua masoko yao.

Waziri Bashe pia ametangaza kuwa Tanzania itasitisha usafirishaji wa mbolea kwenda Malawi kama sehemu ya hatua za kujibu vikwazo hivyo, akitoa notisi kwa wafanyabiashara wa Kitanzania kuwa wasipakie mizigo yoyote kuelekea Malawi kuanzia Jumatano wiki ijayo, iwapo hakutakuwa na mabadiliko ya msimamo kutoka nchi hizo.

“Ifahamike kwamba kama Waziri mwenye dhamana, nimefanya jitihada zote za kuwasiliana na Waziri wa Kilimo wa Malawi, bila kupata majibu yoyote,” amesema.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!