Latest Posts

TANZANIA YAKUBALI KUILIPA INDIANA TSH. BILIONI 237 MGOGORO MRADI WA MADINI YA NIKELI

Serikali ya Tanzania imekubali kuilipa kampuni ya Australia, Indiana Resources Limited fidia ya Dola milioni 90 za Marekani (sawa na Sh237 bilioni), baada ya kuafikiana kutokana na kusitishwa leseni ya mradi wa Ntaka Hill Nickel wa madini ya sulfidi ya nikeli ulioko mkoani Lindi.

Katika taarifa iliyotolewa Julai 29, 2024 na kampuni hiyo imeeleza kuwa uamuzi huo ulitolewa Julai 26, 2023 na Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) ambapo awali uliitaka Tanzania kulipa fidia ya Dola milioni 109 za Marekani (zaidi ya Sh 286 bilioni za kitanzania), baada ya kujiridhisha uwepo wa ukiukwaji wa mkataba wa uwekezaji katika mradi wa Nikeli wa Ntaka Hill mwaka 2018.

Aidha tayari Tanzania imeshalipa dola milioni 35 (sawa na shilingi bilioni 92) kisha watalipa Dola million 25 (sawa na shilingi bilioni 65) kabla ya Oktoba 25 2024 huku kiasi kilichobaki cha dola milioni 30(sawa na Shilingi bilioni 78) kikitarajiwa kulipwa kabla au siku ya tarehe 30 Machi 2025.

“Tanzania itahitajika kukamilisha kiasi kilichobaki katika awamu mbili, Dola milioni 25 ifikapo Oktoba 25, 2024 na Dola milioni 30 ifikapo Machi 30, 2025.

Mgogoro kati ya Indiana Resources na Tanzania ulitokana na mabadiliko ya Sheria za Madini za Tanzania mwaka 2017 na 2018. Januari 10, 2018, kupitia kanuni zake za Haki za Madini za 2018, Tanzania ilitangaza kuwa leseni zote za uhifadhi zilizotolewa kabla ya tarehe ya kuchapishwa kwa kanuni hizo zilifutwa na zitakoma kuwa na athari za kisheria.

Leseni hizo zilikoma kuwa na athari yoyote ya kisheria. Haki za maeneo yote yaliyokuwa chini ya leseni hizo ikiwa ni pamoja na leseni iliyokuwa kwa Indiana Resources zilihamishiwa kwa Serikali. Hali hiyo iliathiri leseni ya uhifadhi ya Indiana Resources kwa mradi wa Ntaka Hill Nickel, uchunguzi na maendeleo ya madini ya sulfidi ya nikeli huko mkoani Lindi na kampuni hiyo ilikadiria thamani ya jumla ya hadi Dola milioni 217.

Leseni za uhifadhi ziliruhusu kampuni kumiliki baadhi ya maeneo yenye madini bila kuendeleza pale ambapo kulikuwa na vikwazo vya kiufundi, hali mbaya ya soko au sababu nyingine za kiuchumi.

Hata hivyo, Serikali ilieleza kuwa utaratibu huo ulikuwa wa kinyonyaji, kwani kampuni zingeshikilia maeneo makubwa bila kuyaendeleza au kuruhusu nchi kupata manufaa yoyote.

Kwa mujibu wa Indiana iliyokuwa ikimiliki asilimia 62.4 ya hisa za kampuni mbili za Ntaka Nickel Holdings Ltd na Nachingwea UK Limited, zilijaribu kuishawishi Serikali kurejesha leseni hiyo, lakini haikufanikiwa hadi mwanzoni mwa mwaka 2020 ndipo ikawasilisha ombi la fidia ICSID ikieleza kupata hasara kubwa za kibiashara kutokana na uamuzi wa Tanzania.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!