Latest Posts

TCB YATUNUKIWA KWA MAGEUZI MAKUBWA YA KIUTENDAJI NA KIUENDESHAJI

Benki ya Biashara Tanzania (TCB) imetunukiwa tuzo kwa kuwa moja ya taasisi zilizofanya mageuzi makubwa ya kiutendaji na kiuendeshaji kama ilivyoonekana katika taarifa yake ya fedha ya robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha (Q1) ambapo ilidhihirisha faida ya kiasi cha Shilingi za Kitanzania bilioni 10.7 ikiwa ni baada ya makato ya kodi.

Utunukiwaji wa tuzo hiyo ulifanyika katika hafla iliyohudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo taasisi na mashirika ya umma yalitoa gawio na michango yao kwa Serikali kama faida ya uwekezaji wa Serikali katika mashirika na taasisi hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TCB, Adam Mihayo ameishukuru Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kuipa TCB nafasi ya kushiriki hafla hiyo huku akiahidi ubunifu zaidi katika sekta ya kibenki ili kuchochea uchumi wa taifa.

“Sisi kama TCB Benki tunaishukuru Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa nafasi hii ya ushiriki na kujionea tukio hili la kitaifa ambalo linatutia nguvu ya kuendeleza safari yetu ya mageuzi ili kuifanya taasisi yetu kuwa benki inayoongoza kwa kuelewa mahitaji ya Watanzania. Ukuaji mkubwa ulioonekana unatokana na dhamira yetu ya kuboresha ufanisi na kuendelea kumridhisha mteja. Katika safari hii ya mafanikio, tunaahidi kuendelea kuwaletea ubunifu wa kifedha unaowezesha ukuaji uchumi na mafanikio ya taifa zima” Amesisitiza Mihayo.

Katika hafla hiyo Serikali ilipokea Shilingi bilioni 637 kama gawio na michango kutoka katika taasisi na mashirika mbalimbali ambapo kati ya fedha hizo, bilioni 279 zilitolewa na mashirika ya kibiashara huku kiasi kilichobaki cha bilioni 358 kikitoka katika mashirika na taasisi nyingine za umma.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu ameeleza kuwa kiasi hicho kilikusanywa kati ya Julai 2023 na Mei 2024 huku jumla ya Shilingi bilioni 850 zikitarajiwa kukusanywa ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni, 2024.

“Jumla ya taasisi 145 zimechangia katika kipindi hiki na hivyo kuongeza idadi kutoka taasisi 109 zilizochangia mwaka jana” Amesema Mchechu.

Aidha amezitaka taasisi ambazo bado zinadaiwa kuhakikisha zinakamilisha michango yao ndani ya mwaka huu wa fedha huku akisisitiza kwamba kuichangia serikali sio jambo la hiari au kujitolea bali ni wajibu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!