Mnada wa nne wa korosho umefanyika leo Novemba 12, 2024 wilayani Tunduru mkoani Ruvuma kupitia Chama Kikuu cha Ushirika (TAMCU) ambapo tani 4,837 za korosho zimeuzwa kwa bei ya wastani ya shilingi 3,290/=
Mnada huo ambao umesimamiwa na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) umefanyika katika kijiji cha Ligoma kata ya Ligoma wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma na kuhudhuriwa na wakulima wa korosho huku bei ya chini ikiwa ni shilingi 3,200/=
Afisa Mwandamizi wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Ezelin Mboma ameeleza kuwa bei za korosho mkoani Ruvuma zimeendelea kuimarika kutokana na wanunuzi wanaoendelea kujitokeza.
“Bei ni nzuri na wakulima wanaendelea kuelewa mfumo huu wa kuendesha minada kidijitali ambao unawapa nafasi ya kushuhudia kila kinachoendelea kutoka kwa wanunuzi,” amesema Mboma.
Katika mnada huo, TAMCU imepeleka sokoni kiasi cha tani 4,837 sawa na kilo 4,837,819 ambazo zote zimenunuliwa.
Kwa upande wake, Meneja wa Bodi ya Korosho Tanzania tawi la Tunduru, Shauri Mokiwa amezungumzia kuendelea kuimarika kwa bei ni kutokana na mazingira mazuri ya minada ya msimu 2024/2025 ambayo yamewekwa na serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wanaoshiriki katika minada ya korosho.
Naye Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika (TAMCU), Mussa Athumani Manjaule amewasisitiza wakulima kuzingatia ubora katika korosho zao, ili zizidi kufanya vizuri pale zinapopelekwa sokoni.
Mohamed Bakari, mkulima wa kijiji cha Ligoma ameeleza kufurahishwa na bei za msimu wa mwaka huu, ambazo amesema zimechangiwa na uwazi uliopo kwenye minada inayosimamiwa na TMX.