News, Njombe.
Vifaa na mahitaji ya zaidi ya Shilingi milioni tatu yamekabidhiwa kwa wanafunzi 120 wenye changamoto ya usikivu katika shule ya sekondari viziwi mkoani Njombe ukiwa ni mchango wa wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika wiki ya shukrani kwa Mlipakodi.
Akikabidhi misaada hiyo Kaimu Meneja wa TRA mkoa wa Njombe Beatrice Kahoho amesema huo ni muendelezo wa kurejesha fadhila kwa jamii katika wiki ya shukrani kwa mlipakodi ili iwasaidie wanafunzi hao wenye mahitaji maalumu kujikimu.
Vifaa vilivyokabidhiwa kwa wanafunzi hao ni pamoja na ‘Projector’ ya kufundishia, mashuka, mafuta, chumvi, sabuni pamona na parachichi kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya lishe.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Viziwi, Mwalimu Rose Mboya ameshukuru kwa msaada huo na kwamba kumekuwa na changamoto kubwa ya mahitaji kwa wanafunzi hao ambao wanatoka familia zenye Uwezo tofauti.
Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi hao wamesema misaada hiyo itakwenda kuwasaidia kupunguza baadhi ya mahitaji hususani kwa watoto wa kike ambao wamepata taulo za kike pia
TRA inatarajia kuhitimisha Wiki ya Shukrani kwa Mlipa Kodi hapo Februari 5 mwaka huu kwa kutoa tuzo mbalimbali kwa wadau na wafanyabiashara waliofanya vyema kwenye sekta ya kodi