Latest Posts

TRA YATANGAZA USHIRIKIANO NA POLISI KUDHIBITI MAGENDO BAADA YA KIFO CHA MTUMISHI WAKE

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Mwenda, ametangaza kuwa oparesheni zote za kitengo cha Fast cha kudhibiti wakwepa kodi zitafanywa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuanzia sasa.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya tukio la kusikitisha la kuuawa kwa dereva wa TRA, Amani Kamguna Simbayao, aliyeshambuliwa na wananchi wakati wa utekelezaji wa majukumu yake katika eneo la Tegeta Nyuki, Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa marehemu, Bw. Mwenda amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuwakamata washukiwa wa tukio hilo na amesisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Amefafanua kuwa gari lililokuwa likifuatiliwa na marehemu na wenzake liliingizwa nchini kwa njia za magendo bila kulipa kodi, na kodi hiyo ingeweza kuchangia maendeleo ya taifa.

“Ningependa mjue kwamba kazi wanayofanya watumishi wa TRA ni kwa niaba ya Watanzania wote. Marehemu Amani alijitahidi kuhakikisha kodi inakusanywa ili kuboresha maisha ya wananchi. Hatustahili kuona wafanyakazi wa TRA wakifanyiwa matendo kama haya. Wanastahili heshima kwa kazi yao kubwa,” amesema Bw. Mwenda.

Amesisitiza kuwa taratibu za usimamizi wa kodi, zikiwemo Sheria za Kodi za Ndani na Sheria za Kiforodha za Afrika Mashariki, zinatoa mamlaka ya kufanya doria, ukaguzi, na ukamataji wa mali zinazohusiana na magendo bila kibali cha mahakama. Kazi aliyoifanya marehemu, alisema, ilikuwa halali na kisheria, lakini ilipingwa kinyume cha sheria na baadhi ya watu waliovunja taratibu.

Bw. Mwenda aliendelea kusema kuwa TRA itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kodi na mamlaka ya watumishi wake katika kutekeleza majukumu yao.

“Kwetu sisi, Marehemu ni shujaa wa taifa. Alifariki akiwa kazini, akilinda mali ya serikali kwa uadilifu na uzalendo mkubwa. Hatutamsahau kwa mchango wake mkubwa,” amesema Bw. Mwenda.

Akizungumzia familia ya marehemu, Bw. Mwenda ameahidi msaada wa kiuchumi na kijamii. Amesema TRA itahakikisha mjane wa marehemu, ambaye ni mjasiriamali, anasaidiwa kupitia mojawapo ya huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo. Watoto wa marehemu pia watapewa bima ya afya ili kuhakikisha wanapata matibabu bila changamoto yoyote.

“Sisi kama TRA tutasimamia kuhakikisha mjane na watoto wake hawaachiwi kuteseka. Tutaendelea kuwa nao katika kila hatua,” ameongeza Kamishna Mwenda

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!