Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa Marekani inatarajia kuanzisha mazungumzo na Iran wiki ijayo, huku akisisitiza kuwa hatarajii tena kuwepo kwa vita kati ya Iran na Israel, kutokana na kile alichokiita kuvunjwa kwa uwezo wa nyuklia wa Iran.
Akizungumza na wanahabari jijini Washington, Trump amesema mazungumzo hayo yana lengo la kutuliza mvutano na kuanzisha enzi mpya ya maelewano. Hata hivyo, aliongeza kuwa hatalazimika kufikia makubaliano iwapo pande zote hazitakuwa tayari.
“Tutazungumza na Iran wiki ijayo, labda tutafikia makubaliano,” amesema Trump na kuongeza: “Lakini mimi sihitaji makubaliano. Walipigana vita, sasa wanarudi kwenye ulimwengu wao wenyewe. Sijali kama kutakuwa na makubaliano au la.”
Akijibu swali kuhusu iwapo Iran ilihamisha nyenzo za nyuklia kabla ya mashambulizi ya Marekani, Trump amesema hilo halikutokea kutokana na uzito na ugumu wa kuhamisha vifaa hivyo. Trump amesisitiza kuwa uwezo wa nyuklia wa Iran kwa sasa umesambaratika kabisa
Kauli yake imeungwa mkono na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, ambaye amesema kuwa Rais Trump yupo tayari kuzungumza na wale wote wanaotafuta amani, lakini akabainisha kuwa hilo litategemea dhamira ya Iran.
Kauli hizi zinakuja wakati ambapo jumuiya ya kimataifa inaendelea kushuhudia mvutano wa mara kwa mara kati ya Iran na Israel, huku wasiwasi wa kuibuka kwa vita kubwa zaidi ukitawala katika Mashariki ya Kati. Marekani, kupitia hatua mbalimbali za kijeshi na kisiasa, imekuwa ikijaribu kudhibiti ushawishi wa Iran katika eneo hilo, hasa kuhusu mpango wake wa nyuklia.