Latest Posts

VIFO 16 VYATOKEA KENYA KATIKA MAANDAMANO YA KUMBUKUMBU YA JUNI 25

Watu 16 wamethibitishwa kufariki dunia kufikia Jumatano usiku, wengi wao wakidaiwa kuuawa kwa risasi na polisi, wakati wa maandamano makubwa nchini Kenya yaliyoandaliwa kuadhimisha mwaka mmoja tangu maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024 uliosababisha uvamizi wa Bunge la Taifa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Amnesty Kenya, Bw. Irungu Houghton, vifo hivyo vimethibitishwa kwa ushirikiano na Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR). “Wengi waliuawa kwa mikono ya polisi, takribani watano walipigwa risasi moja kwa moja,” amesema Houghton.

Katika maandamano hayo yaliyofanyika jijini Nairobi na miji mingine ikiwemo Mombasa, Kitengela, Kisii, Nyeri na Matuu, polisi walitumia mabomu ya machozi, maji ya kuwasha, risasi za mpira na silaha za moto kuwatawanya waandamanaji.

KNCHR iliripoti kuwa watu zaidi ya 400 walijeruhiwa, wakiwemo waandamanaji, polisi na wanahabari. Tume hiyo ilibainisha kuwa waathirika wengi walijeruhiwa kwa risasi halisi au za mpira.

Kwa upande wake, Msemaji wa Polisi Muchiri Nyaga alikataa kutoa maoni kuhusu tuhuma hizo. Hata hivyo, Mamlaka ya Usimamizi wa Polisi Huru (IPOA) ilithibitisha kukamatwa kwa watu 61 wakati wa maandamano.

Katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), afisa mmoja alieleza kuwa wamepokea majeruhi zaidi ya 100, wengi wakiwa na majeraha ya risasi. “107 wamepokelewa, wengi wakiwa na majeraha ya risasi halisi au za mpira,” amesema.

Katika tukio la kusikitisha, shirika la Kenya Power liliripoti kuwa mlinzi wao mmoja alipigwa risasi na kuuawa akiwa kazini katika makao makuu ya shirika hilo jijini Nairobi.

Katika hali ya taharuki, waandamanaji walionekana wakielekea Ikulu ya Nairobi (State House), kabla ya vituo viwili vya televisheni—NTV na KTN—kufungiwa kwa kukaidi agizo la mamlaka ya mawasiliano (CAK) la kusitisha matangazo ya moja kwa moja. Hata hivyo, mahakama ilisitisha agizo hilo baadaye na vituo hivyo vikaendelea kurusha matangazo.

Maandamano haya yanakuja katika kipindi ambacho raia wengi wa Kenya wanaendelea kulaani vitendo vya polisi kutumia nguvu kupita kiasi, hasa baada ya kifo cha mwalimu na mwanablogu Albert Ojwang, ambaye alifariki akiwa rumande mwezi huu.

Jumanne, polisi watatu na watu wengine watatu walifikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa mauaji ya Ojwang. Wote walikana mashtaka hayo.

Ojwang, aliyekuwa akiandika kuhusu madai ya ufisadi dhidi ya Naibu Mkuu wa Polisi, Eliud Lagat, alifariki katika hali ya kutatanisha, kifo chake kikigeuka kuwa kiini cha hasira ya umma na kuibua kumbukumbu chungu za waliopoteza maisha mwaka jana.

“Tunapigania haki za vijana wenzetu, haki za Wakenya wote na wale waliouawa tangu Juni 25. Tunataka haki itendeke,” alisema Lumumba Harmony, mmoja wa waandamanaji jijini Nairobi.

Tukio la mwaka jana, ambapo waandamanaji walivamia Bunge la Taifa na kupigwa risasi na polisi, lilikuwa mtihani mkubwa zaidi wa uongozi wa Rais William Ruto na liliibua tahadhari miongoni mwa washirika wa kimataifa wa Kenya.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!