Kampuni ya Vivo Energy Tanzania, inayosimamia vituo vya mafuta vya Engen na Shell, imezindua kampeni mpya inayolenga kusaidia wanafunzi wa shule za serikali na binafsi kwa kuhakikisha wanapata usafiri wa uhakika kwenda shuleni. Kampeni hiyo inaitwa “Safari ya Elimu, Kata Kilometa kwa Uhakika”
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo Ijumaa, Januari 31, 2025, katika eneo la Masaki, Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Masoko, Mawasiliano na Miradi ya Kijamii wa Vivo Energy Tanzania, Aileen Meena, amesema kuwa mpango huu unalenga kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekosa masomo kwa sababu ya changamoto za usafiri.
“Wanafunzi wasiache kwenda shule kisa bajaji imekosa mafuta au haijafanyiwa huduma. Kupitia kampeni hii, tutatoa mafuta ya nyongeza kwa vyombo vya usafiri vinavyobeba wanafunzi, ikiwemo mabasi ya shule na bajaji, katika vituo vya Engen vilivyopo Kinondoni, Masaki na Mbezi Beach,” amesema Meena.
Ameongeza kuwa lengo la kampeni hiyo ni kusaidia wanafunzi na kuwahamasisha wadau wa sekta binafsi kushiriki katika kusaidia elimu.
“Tunasema elimu ni kila kitu. Hata wamiliki wa daladala na waendeshaji wa bajaji wanaweza kutoa ofa kwa wanafunzi waliokosa nauli, kwa sababu huwezi kujua, huenda unamsaidia Rais wa kesho, Mkurugenzi au mfanyabiashara mkubwa,”* amesisitiza.
Katika kampeni hiyo, mtu yeyote anayebeba mwanafunzi na kununua mafuta na kilainishi cha Shell kwenye vituo vya Engen vilivyochaguliwa ataongezewa mafuta pamoja na zawadi kwa mwanafunzi.
“Hii ni fursa adhimu kwa madereva wa vyombo vya usafiri kusaidia wanafunzi katika safari yao ya elimu. Tunatoa rai kwa Watanzania wote kutumia biashara zao kusaidia watoto kwa namna wanavyoweza ili kujenga msingi wa kesho,”* amehitimisha Meena.