Wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu mkoani Dar es Salaam wametoa tamko rasmi kuunga mkono azimio la Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumteua Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Dkt. Hussein Ally Mwinyi kuwa mgombea wa urais wa Zanzibar kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Tamko hilo limetolewa katika ofisi za Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoa wa Dar es Salaam na Pascrates Albinus Mwemezi, Mwenyekiti Wa UVCCM Seneti ya Vyuo na Vyuo Vikuu Mkoa wa Dar Es Salaam, na Mabula Marco Mabula, Katibu wa UVCCM Seneti ya Vyuo na Vyuo Vikuu Mkoa wa Dar Es Salaam
Wakizungumza kupitia tamko hilo, viongozi hao wamesema uteuzi wa Dkt. Samia na Dkt. Mwinyi ni matokeo ya kazi kubwa waliyoifanya katika nyanja mbalimbali, hasa kwenye sekta ya elimu.
“Rais Samia amethibitisha kuwa ni mlezi wa kweli wa vijana, haswa sisi wanavyuo. Itakumbukwa Februari 11, 2022, alikutana na viongozi wa serikali za wanafunzi Ikulu ya Chamwino kusikiliza changamoto zetu na kuzitafutia ufumbuzi. Hatua hii ilionyesha kujitolea kwake kwa dhati katika kuboresha elimu ya juu,” wamesema.
Katika tamko hilo, wamebainisha mafanikio kadhaa chini ya uongozi wa Dkt. Samia, ikiwemo ongezeko la bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambayo imepanda kutoka TZS bilioni 570 mwaka 2021/2022 hadi TZS bilioni 787 mwaka 2024/2025, huku idadi ya wanufaika ikiongezeka kutoka 177,892 hadi 245,799. Vilevile, kiwango cha fedha za kujikimu kwa siku kwa wanafunzi kimeongezwa kutoka TZS 8,500 hadi TZS 10,000 kwa mwaka wa masomo wa 2023/2024.
Aidha, tamko hilo limesisitiza juhudi za serikali katika ujenzi wa miundombinu ya elimu, ikiwemo madarasa 23,000 yaliyokamilika nchi nzima, ujenzi wa kampasi 14 za vyuo vikuu kupitia mradi wa HEET, na ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi (VETA) katika kila wilaya.
Kwa upande wa Dkt. Hussein Mwinyi, viongozi hao wamempongeza kwa juhudi zake katika kuimarisha sekta ya elimu Zanzibar, wakibainisha kuwa uongozi wake umejikita katika kuhakikisha vijana wanapata nafasi sawa za masomo na kujiajiri.
Aidha wametangaza kuwa wamesaini kitambaa maalum cha kuunga mkono uteuzi wa wagombea hao wa CCM na kuahidi kuwashawishi wenzao kuwachagua katika uchaguzi wa 2025.
“Kwa pamoja tunasema, Dkt. Samia na Dkt. Mwinyi ni viongozi wenye dira na maono makubwa kwa maendeleo ya Tanzania na Zanzibar. Tunawahakikishia kura zetu kwa asilimia 100,” amesema mmoja wa viongozi hao.