Latest Posts

WAJIFANYA VIONGOZI NA KUTAPELI MILIONI TANO, WALIZA WASTAAFU

Watuhumiwa wanne kutoka mikoa Kagera na Mwanza, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka 49 ikiwemo kuendesha genge la uhali na kutapeli watu kwa njia ya simu, kujitambulisha kama viongozi kisha kujipatia fedha Sh. Milioni tano 5,000,000/= pamoja na kuwadanganya wastaafu kuwa watawapatia mafao yao.

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali Mwandamizi Nura Manja imewataja washtakiwa hao kuwa ni Eradius Rwechungura (43), mfanyabiashara mkazi wa Kiseke Mwanza, Heri Kabuju maarufu kama Babylon (37), Mvuvi mkazi Rwamisheni Kagera, Abdurahim Karugula maarufu kama Obra (42), dereva na anaishi Kahoro Kagera na Eradius Apornary (22), mkazi wa Kashai Kagera

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki washtakiwa hao wamesomewa mashtaka 49 kati ya hayo, mashtaka 23 ya kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, mashtaka 13 ya kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa majina ya mtu mwingine, mashtaka 11 ni ya kujitambulisha kwa utambulisho wa mtu mwingine, shtaka moja la kuongoza genge la uhalifu na shtaka la mwisho la utakatishaji fedha.

Mshtakiwa wa kwanza Rwechungura peke yake anakabiliwa na mashtaka mawili ya kutoa utambulisho usio wake, matatu ya kutumia laini iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine na mashtaka saba ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu wakati mshtakiwa Kabaju yeye anamashtaka sita ya utambulisho usio wake, mawili ya kusajili laini jina kwa kutumia jina la mtu mwingine na mashtaka 11 ya kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu.

Mshtakiwa wa pili Karugula anamashtaka matatu ya utambulisho usiokuwa wake, matano ya kutumia laini iliyosajiliwa kwa jina jina la mtu mwingine na mashtaka sita ya kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu huku mshtakiwa Apornary akikabiliwa na mashtaka matatu ya kutumia laini ya simu  yenye jina la mtu mwingine mwinigine.

Katika shtaka la kwanza inadaiwa kati ya Oktoba Mosi na Desemba 31,2024 eneo lisilojulikana nchini Tanzania washtakiwa wote kwa pamoja waliendesha genge la uhalifu kwa lengo la kutapeli watu tofauti tofauti na kujiwasilisha uongo kwa watu mbakimbali na kujipatia shilingi milioni tano 5,000,000/=.

Mshtakiwa Rwechungura anadaiwa kujitambulisha kuwa ni Afisa kutoka Idara ya Rasilimali Watu katika Ofisi ya Katibu Tawala Wilaya ya Bukoba kwa Eliberth Kalima na kuwa ni Afisa kutoka Ofisi ya Mkurugenzi katika Halmashauri ya Kahama mjini kwa Filberth Mashim huku akijua si kweli.

Pia Kabuja anadaiwa kuwadanganya wastaafu kwa kujitambulisha kuwa yeye Afisa kutoka Mfuko wa Hifadhi wa Jamii PSSSF kwa Anunciata Mwageni pia alijitambulisha kuwa ni Afisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kupata taarifa za muajiriwa Christopher Msemwa pia alidai kuwa ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe kwa Jesca Kibena.

Aliendelea kudai kuwa Kabuja alijitambulisha kuwa ni Afisa Rasilimali watu kutoka ofisi ya Halmashauri ya Njombe mjini kwa Rustica Kayombo na Upendo Nsellu pia alijiwasilisha kama Mweka Hazina wa Idara ya Pensheni kwa Lucas Nzota na kuwa angemsaidia kupata mafao yake huku akijua kuwa si kweli.

Aidha washtakiwa wanadaiwa walikuwa wakitumia laini zilizosajiliwa kwa majina ya Bazil Katono, Happyness Jems, Aziza Ramadhani, Royce Frank, Sajda Abed, Valence Rwezaula, Ben Mhimbira, Benetson Rwenyagira na Sabitina Ally.

Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi ambazo kwa kawaida husikilizwa mahakama Kuu ama kwa kupewa kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi bado haujakamilika na kesi imeahirishwa hadi Februari 14, mwaka huu. Washtakiwa wote wamerudishwa rumande.

 

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!