Usiku wa Desemba 06.2024, Alhamisi Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kiliandaa hafla maalum ya kukutana na wawekezaji mahiri na wawekezaji mahiri maalum (wawekezaji wazito), tukio lililofanyika Serena Hotel, jijini Dar es Salaam
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo aliyekuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo amesema wawekezaji mahiri na wawekezaji mahiri maalum ni wale wawekezaji waliowekeza Tanzania kwa mtaji usiopungua dola za Kimarekani milioni 20 ambayo ni sawa na takribani shilingi bilioni 60 za Kitanzania
Prof. Kitila amesema pamoja na mambo mengine lakini lengo la kuandaliwa kwa hafla hiyo iliyohusisha wawekezaji wa ndani na nje ya Tanzania, ni pamoja kuwasikiliza na kuelezana mafanikio yaliyopatikana mwaka huu (2024), sambamba na kuelezana ajenda zinazokuja siku za usoni kuanzia mwakani (2025) na kuendelea
“Mchango wa watu hawa ni mkubwa, kwa sababu tunapozungumzia uchumi maana yake ni uwekezaji na bila ya uwekezaji hakuna uchumi, wawekezaji wakiwekeza ndio biashara zinafanyika, biashara zikifanyika ndipo ajira zinavyozalishwa, zikizalishwa ajira tunapata kazi, tunapata mitaji, tunapata teknolojia kwa hiyo wawekezaji ni muhimu sana kwenye uchumi, bila uwekezaji huwezi kuzungumzia uchumi wowote” -Prof. Kitila
Akizungumzia hafla hiyo, Mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Gilead Teri amesema sheria ya uwekezaji nchini inatambua kuwa wawekezaji mahiri na wawekezaji mahiri maalum ni wale wanaowekeza zaidi ya dola za Kimarekani milioni 20 kwa Mtanzania na dola za Kimarekani milioni 50 kwa wawekezaji wanaotoka nje ya nchi, na ikumbukwe dola milioni 50 za Kimarekani zinazozungumzwa ni uwekezaji wa zaidi ya bilioni 100 kwenye mradi mmoja
Amesema wawekezaji waliokutananao ni kati ya 50 hadi 60, ambapo moja ya mijadala iliyoangazwa kwenye hafla hiyo ni pamoja na kufahamu uwekezaji wao umefikia wapi ili kuona kama kuna changamoto zozote wanazokutananazo zitafutiwe ufumbuzi, sambamba na kuwaeleza kama kuna maboresho yoyote yanayotarajiwa kufanya kuanzia mwakani (2025)
“Kama ingekuwa biashara hawa ndio wafanyabishara wetu wakubwa, ndio wanaoajiri watu wengi, ndio wanaolipa kodi kubwa, ndio wanaochangia kuleta teknolojia mpya kwenye uchumi wetu, kwa hiyo ni watu wa maana na watu wa kuwathamini, lakini pia sio wawekezaji wa nje pekee bali wako Watanzania wengi tu ambao ni wawekezaji mahiri na mahiri maalum” -Teri