Aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, Ezekiah Wenje, amewapongeza Mwenyekiti mpya wa CHADEMA, Tundu Lissu, na Makamu Mwenyekiti Bara, John Heche, kwa ushindi wao katika uchaguzi wa chama hicho.
Kupitia chapisho lake kwenye mtandao wa X, Wenje ameandika:
“Watu wetu wamezungumza: Nakupongeza sana Tundu Lissu na ndugu yangu Heche kwa ushindi. Tutawapa ushirikiano pamoja na ‘check and balance’. Kwa walioniunga mkono pamoja na timu yangu ya kampeni, Mungu awabariki sana. Freeman Mbowe, wewe ni nembp ya demokrasia yetu”.
Wenje amesisitiza dhamira yake ya kutoa ushirikiano kwa viongozi wapya huku akiwahakikishia kuwa atafanya kazi ya kuhakikisha uwajibikaji katika chama.
Aidha, amempongeza Freeman Mbowe, aliyemaliza muda wake wa uongozi, kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha demokrasia nchini, akimuelezea kama “nembo ya demokrasia.”
Ushindi wa Lissu na Heche umeendelea kupongezwa na viongozi wa ndani na nje ya CHADEMA, ukitafsiriwa kama hatua muhimu katika harakati za chama hicho kuimarisha demokrasia nchini Tanzania.