Asasi za kiraia za Afrika, zikiwemo za Tanzania, zimeitaka jumuiya ya kimataifa kufanya mageuzi makubwa ya mfumo wa fedha wa dunia ili kuondoa ukosefu wa usawa, madeni kandamizi, na mifumo ya uchumi inayowanyima watu haki ya maendeleo.
Wito huo umetolewa Julai 3, 2025 katika Mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu Ufadhili kwa Maendeleo (FFD4) unaofanyika Seville, Hispania kuanzia Juni 30 hadi Julai 3, 2025, ambapo viongozi wa dunia, taasisi za kifedha, mashirika ya kiraia na wadau wa maendeleo wanajadili njia za kufadhili maendeleo endelevu.
Mkutano huo unakuja wakati dunia ikikabiliwa na migogoro ya madeni, athari za mabadiliko ya tabianchi, na pengo kubwa la kiuchumi kati ya mataifa tajiri na maskini.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mtandao wa Kutokomeza Umasikini Duniani (GCAP), umaskini barani Afrika si ajali, bali ni matokeo ya mifumo ya kiuchumi isiyo ya haki.

“Tunahitaji haki, si hisani. Rasilimali na fedha lazima zitumikie watu wengi, si wachache,” amesema
Katika msimamo wao wa pamoja, mashirika ya kiraia yamependekeza hatua saba za kipaumbele ambazo ni pamoja na:
Kufutwa kwa madeni yasiyo halali na kuelekeza fedha hizo kwenye huduma za jamii kama afya, elimu na miradi ya maendeleo;
Mageuzi ya mfumo wa fedha wa kimataifa, hususan Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, ili mataifa ya Afrika yashiriki kwa usawa katika uamuzi wa sera;
Kuzuia ukwepaji kodi na uhamishaji haramu wa fedha, ambapo Afrika hupoteza zaidi ya dola bilioni 88.6 kila mwaka;
Kuongeza thamani ya rasilimali ndani ya Afrika, badala ya kuuza malighafi kwa bei ya chini na kununua bidhaa zilizosindikwa kwa gharama kubwa;
Ufadhili wa mapambano dhidi ya tabianchi kwa njia ya ruzuku, si mikopo, ikizingatiwa kuwa Afrika huchangia chini ya asilimia 3 ya hewa chafu lakini huathirika zaidi;
Kujenga uchumi imara na huru, kupitia usimamizi bora wa madini, kilimo, bahari na utalii;
Utawala wa dunia wa kidemokrasia, unaowapa Waafrika nafasi ya kutunga sera, si kupokea maagizo pekee.
Wawakilishi wa asasi za kiraia kutoka Tanzania wamesema kuwa mfumo wa sasa wa fedha wa kimataifa umechangia kudhoofisha maendeleo ya kweli na kuendelea kutegemea madeni.

“Nchi nyingi zinatumia fedha nyingi kulipa madeni kuliko kwa huduma za msingi kama afya na elimu. Tunataka rasilimali zetu zitumike kwa maendeleo ya watu wetu,” amesema
FFD4 ni muendelezo wa mikutano iliyofanyika Monterrey (2002), Doha (2008), na Addis Ababa (2015), inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika ufadhili wa maendeleo, hususan katika kutokomeza umaskini na kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Kwa mara nyingine, Afrika imeonesha mshikamano katika kudai mfumo mpya wa kifedha wa kidunia unaozingatia usawa, uwajibikaji, na haki za binadamu.
“Hii si misaada ni haki. Haki ya maendeleo ni haki ya binadamu,” wanasema kwa pamoja wawakilishi wa mashirika ya kiraia kutoka bara la Afrika.
