Latest Posts

JESHI LA POLISI LALAUMIWA KWA UKANDAMIZAJI WA WANACHAMA WA UPINZANI

Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuingilia kati haraka ili kukomesha ukiukwaji wa haki za binadamu unaodaiwa kufanywa na Jeshi la Polisi nchini.

ACT kupitia taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari siku ya Jumamosi Desemba 07, 2024 na Naibu Katibu wa Haki za Binadamu wa chama hicho, Mbarala Maharagande, kimesisitiza kuwa vitendo vya ukandamizaji vinavyofanywa dhidi ya wanachama wake na raia wengine ni tishio kwa misingi ya demokrasia na utawala wa sheria.

Katika taarifa yake, ACT Wazalendo imetaja vitendo vya vitisho, utesaji, ukamataji holela, na kupigwa kwa wanachama wake kama sehemu ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliotokea katika kipindi cha uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji uliofanyika tarehe 27 Novemba 2024.

ACT Wazalendo imebainisha kuwa Jeshi la Polisi limekuwa likilenga wanachama wake katika matukio mbalimbali nchini, yakiwemo wanachama wake saba kukamatwa Kata ya Ruhuhu mkoani Njombe, kupigwa na kulazimishwa kuvaa sare za chama chao kabla ya kuchukuliwa na polisi.

ACT imesema kuwa tukio lingine ni la huko Kigoma Kaskazini na Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma ambapo wanachama kumi na wanawake saba wenye watoto wadogo walikamatwa kwa madai ya kuharibu nyaraka za uchaguzi. Aidha, zaidi ya wanachama 200 walikimbia makazi yao kutokana na vitisho na mashambulizi.

Lakini pia Kasulu Vijijini mkoani Kigoma, Diwani wa Kata ya Rungwe Mpya, Jonas Abel Kaja, alikamatwa kwa tuhuma za kuhusika na tukio la kumwagia tindikali kiongozi wa CCM, ingawa chama hicho kinapinga madai hayo.

Chama hicho kimeeleza kuwa Jeshi la Polisi limekuwa likipendelea upande wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwalinda wahalifu wanaohusishwa na chama hicho huku likiwabambikizia kesi wanachama wa upinzani kikitoa mifano ya kupigwa na kuumizwa kwa viongozi wa ACT Wazalendo, ikiwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Mkoa wa Songwe na Katibu wa Jimbo la Igunga.

Aidha matukio mengine ni kuporwa mali, kama ilivyotokea kwa binti wa mgombea wa kijiji cha Mgomba Kati, ambaye alipigwa vibaya na makada wa CCM huku polisi wakiwataka wahalifu waende hospitali kuomba msamaha badala ya kuchukuliwa hatua za kisheria, na tukio la hivi karibuni lililomhusisha mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa chama hicho taifa Abdul Nondo ambaye alielezwa kutekwa.

Kutokana na matukio hayo miongoni mwa mengine iliyoyaeleza katika taarifa yake, ACT imemtaka Rais Samia Suluhu Hassan kuviamuru vyombo vya dola kusitisha mara moja uonevu wa kisiasa unaofanyika kwa kutumia vibaya madaraka yao.

Aidha imetaka kuachiliwa huru kwa viongozi na wanachama wa ACT Wazalendo wanaoshikiliwa bila kufikishwa mahakamani, Jeshi la Polisi kuacha upendeleo wa kisiasa na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria bila kupendelea chama chochote, na jumuiya ya kimataifa na wadau wa demokrasia kuingilia kati kwa kutoa presha kwa serikali ili kuheshimu haki za binadamu na uhuru wa kisiasa.

ACT Wazalendo imesisitiza kwamba matumizi ya vyombo vya dola kama chombo cha kukandamiza siasa za upinzani hayatakomesha mapambano ya kudai haki, usawa na demokrasia nchini. Chama hicho pia kimeendelea kuunga mkono harakati za kudai Katiba Mpya na mabadiliko ya sheria za uchaguzi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!