Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu leo, tarehe 22/07/2026 amemuhoji maswali ya dodoso (cross examination) shahidi wa Nne (4) katika shauri la Kikatiba Na. 7300/2026 linaloendelea kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu Dodoma, inayoketi vikao vyake kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam mbele ya jopo la Majaji watatu watatu (3) wakiongozwa na Jaji Amir Mruma.
Shahidi huyo ambaye kimsingi ni shahidi wa kwanza na pekee wa Jamhuri katika shauri hilo lililofunguliwa na Mawakili watatu (3) ambao ni Kulwa William Maduhu, Nashon Nkung na Paul Kisabo dhidi ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Nchini (CGP) na wenzake wanne (4), ni Mkuu wa Gereza la Ukonga, Dar es Salaam ACP Andrew Shaban N’tamamiro
Katika maswali yake ya dodoso, pamoja na mambo mengine Lissu ambaye anajiwakilisha mwenyewe amemuhoji shahidi huyo endapo ni kweli au si kweli kwamba kwenye masuala yanayomuhusu yeye (Lissu) amekuwa akiendesha ‘kwa rimoti’ na Mlalamikiwa wa pili (2) kwenye shauri hilo ambaye ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Nchini (CGP) na wanasiasa walioko Serikalini, hata hivyo shahidi huyo alijibu kuwa si kweli
Baada ya kujibiwa hivyo, Lissu ambaye kitaaluma ni Mwanasheria na Wakili mbobevu alitoa mifano aliyodai kuwa inahusiana moja kwa moja na kile alichozungumza Mahakamani hapo kwamba Mkuu huyo wa Gereza Ukonga amekuwa akiendeshwa kwa ‘rimoti’ na CGP na wanasiasa walioko Serikalini hasa kwenye mambo yanayomuhusu yeye (Lissu)
Amedai kuwa siku moja aliitwa kwenye Ofisi ya shahidi huyo na kuelezwa kuwa kuna ujumbe muhimu umetumwa gerezani kwamba Lissu anatakiwa kwenda mjini kukutana na Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, ambaye ni Rais Mstaafu wa Malawi Dkt. Lazarus Chakwera, na ilikuwa hivyo
Anasema mara nyingine, ni pale alipomuita tena Ofisini kwake na kumueleza kuwa anatakiwa kwenda mjini kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Martin Chungong, na ilikuwa hivyo Lisuu alienda Mjini akiwa anasindikizwa na mmoja wa maafisa wa Magereza
Amedai kuwa, mara nyingine ni pale alipowafungulia na kuwaingiza gerezani Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania Bara John Heche, Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania Bara Amani Golugwa, ili wakazungumze na yeye (Lissu) kuhusiana na mambo fulani ambayo msingi wake ulitokanana na msukumo kutoka kwa ‘wanasiasa serikalini’, Lissu anadai kwamba viongozi hao wa CHADEMA waliruhusiwa kuingia gerezani katika wakati ambao kuna marufuku ya kuwazuia wasifike kumuona lakini kwa siku hiyo iliwezekana
Hata hivyo, madai yote hayo yalikanushwa vikali na shahidi huyo, na kila swali alilokuwa anaulizwa kwenye eneo hilo na hata lile la kuwpaiga marufuku viongozi na makada wa CHADEMA kufika gerezani kumuona yote alijibu ‘Si Kweli’
Maeneo mengine aliyogusia Lissu kwenye maswali yake ya dodoso ni kuhusu kuzuiliwa kufika gerezani kwa baadhi ya Mawakili wake ambao pia ni viongozi wa CHADEMA kama vile Dickson Matata, Deogratias Mahinyila na Gaston Garubindi
Kukosekana kwa faragha kwenye mazungumzo baina yake na Mawakili wake, hata hivyo madai yote hayo yalikanushwa vikali na shahidi huyo,
Shauri hilo limeahirishwa hadi kesho, tarehe 23/07/2026 ambapo Mawakili wa waleta maombi wakiongozwa na John Seka, na Wakili Emmanuel Ukashu anayewakilisha Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) wataendelea kumuhoji maswali yao ya dodoso (cross examination).