Shauri la Kikatiba Na. 7300/2026 lililofunguliwa na Mawakili Kulwa William Maduhu, Nashon Nkung na Paul Kisabo dhidi ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Nchini (CGP), Mkuu wa Gereza Ukonga, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Tundu Lissu limeendelea leo, Alhamisi tarehe 23/07/2026, Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu Dodoma inayoketi vikao vyake kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam
Shauri hilo linalosikilizwa na jopo la Majaji watatu (3) wakiongozwa na Jaji Amir Mruma limekuja Mahakamani hapo leo mahsusi kwaajili ya shahidi pekee wa Jamhuri, Mkuu wa Gereza Ukonga ACP Andrew Shaban N’tamamiro kuendelea kuhojiwa maswali ya dodoso (cross examination) kutoka kwa wadaawa wengine, baada ya mjibu maombi wa Nne (4) kwenye shauri hilo Tundu Lissu kumaliza kuhoji maswali yake jana, tarehe 22/07/2026
Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ambao ni wadaawa wenye maslahi kwenye shauri hilo jopo lao uwakilishi limeongozwa na Wakili Emmanuel Ukashu, ambapo katika maswali yake ya dodoso alianza kwa kumuuliza shahidi huyo ambaye kimsingi ni mjibu maombi wa pili (2) kwenye shauri hilo kwamba katika utumishi wake wa miaka 31 ndani ya Jeshi la Magereza anafahamu kitu gani kuhusu TLS?, shahidi huyo alijibu kuwa amekuwa akisia tu
Alipoulizwa endapo anafahamu au hafahamu kama waleta maombi wote watatu (3) kuwa ni Mawakili, shahidi huyo alijibu kuwa ni sahihi, hata hivyo alipoulizwa swali kama hilo kuhusu mjibu maombi wa Nne (4) ambaye ni Tundu Lissu, shahidi alisema hajuwi
Wakili Emmanuel Ukashu alienda mbali zaidi na kumuuliza shahidi huyo endapo anafahamu au hafahamu kuwa mjibu maombi wa Nne (4) Tundu Lissu amewahi kuwa Rais wa TLS kwa kipindi cha mwaka mmoja (2017/18), na kwamba hata hivyo alishindwa kukamilisha kipindi chake cha uongozi kufuatia kushambuliwa kwa risasi mwaka 2017, majibu ya shahidi kwenye eneo hilo yalikuwa ni kwamba hafahamu
ACP Andrew Shaban N’tamamiro, Mkuu wa Gereza Ukonga ambaye kwa ujumla wake ni shahidi wa Nne (4) katika orodha ya mashahidi waliopanda kuzimbani kuhusiana na shauri hilo, aliulizwa pia anaelewa nini anaposikia maneno ‘maagizo kutoka juu’, na katika majibu yake alieleza kuwa tafsiri ya uelewa wake ni maagizo ya kiutendaji
Hata hivyo alipoulizwa endapo, anaweza kupokea au kukataa maelekezo yanayotoka kwa mabosi zake wa juu ikiwemo Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Nchini (CGP), shahidi huyo alijibu kuwa hawezi kumbishia, hata hivyo alikanusha madai kwamba endapo akibishia anaweza kufukuzwa kazi moja kwa moja kutokana na kile alichoeleza kuwa zipo taratibu za kufuatwa kabla ya maamuzi hayo,
Mapema leo, Mawakili wa waleta maombi John Seka na Edson Kilatu, kwa nyakati tofauti nao walimuohoji maswali ya dodoso shahidi huyo, ambao miongoni mwa maswali waliyomuuliza ni yale yanayohusu maelezo yaliyotolewa na mashahidi waliomtangulia Mahakamani hapo kuhusu sehemu walizofanyia mazungumzo na mteja wao pindi walipoenda kumtembelea gerezani, hoja ambazo hakuzikanusha
Hata hivyo, alipoulizwa mazingira ya namna ya ukaaji kwamba zilikuwa meza tatu za watu wanaoandika, na kwamba Mawakili walilazimika kukaa hapo pia shahidi huyo alijibu ‘ndio’, hata hivyo alivyotakiwa kukadiria ukubwa wa meza hizo shahidi alisema hajuwi
Alipoulizwa endapo aliwahi kumuona au kumfahamu mleta maombi wa kwanza (1) Kulwa William Maduhu, shahidi alijibu hapana, lakini kuhusu waleta maombi wengine yaani Nashon Nkung na Paul Kisabo aliieleza Mahakama kuwa hao anawafahamu
Alipotakiwa kueleza namna alivyowafahamu watu hao, alijibu kuwa amekuwa akiwaona mara kwa mara wanapokwenda gerezani kumuona mteja wao Tundu Lissu, hata hivyo madai ya kuwahi kukutana na Mawakili hao Ofisini kwake, lakini amekiri kuwa amewahi kukutananao Ofisi ya Bwana Recha na admission office
Alipoulizwa endapo amewahi kuhudhuria mazungumzo baina ya Mawakili hao na mteja wao Tundu Lissu, shahidi huyo alikana, badala yake alikiri kuwa amewahi kuchungulia wanapokuwa wamekaa
Kuhusu suala la maafisa wa Jeshi la Magereza kuwazunguka na kuwasikiliza Lissu na Mawakili wake wakiwa kwenye mazungumzo ya faragha, shahidi huyo alikanusha madai hayo na kuieleza Mahakama kuwa wakati wao wanazungumza askari na wahusika wengine wa Ofisi wanakuwa nje lakini mlango wa chumba wanachotumia kwa mazungumzo unakuwa wazi ili waweze kuwaona, na si kuwasikia
Baada ya kukamilika kwa maswali ya dodoso (cross examination), Mahakama ilitoa nafasi kwa Mawakili wa Jamhuri kumuhoji shahidi Re-Examination, zoezi ambalo halikuchukua muda mrefu hadi kukamilika kwake, na kesi hiyo sasa imeahirishwa hadi tarehe 16/09/2026 itakapotajwa tena Mahakamani, huku kipindi cha kati kabla ya tarehe husika pande zote zikiwasiliana kwa maandishi kufuatia mapingamizi yaliyowekwa na waleta maombi
Ikumbukwe kuwa, msingi wa shauri hilo ni waleta maombi ambao wamejitambulisha kuwa ni Mawakili wa Tundu Lissu kulalamikia kuzuiwa na/au kunyimwa faragha ya kuzungumza na mteja wao pindi wanapomtembelea Gerezani jambo ambalo wamedai kuwa ni kinyume cha taratibu, sheria, kanuni na uvunjifu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977.