Vijana wa Kikundi cha Smart Boda cha Ikina kilichopo Kata ya Bukoli, Jimbo la Busanda, wamepokea mkopo wa pikipiki 10 zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 20 kupitia mpango wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa lengo la kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi.
Mkopo huo umetolewa kupitia mfuko wa mikopo usio na riba kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, ukiwa sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kukuza uchumi wa wananchi kupitia uwezeshaji wa makundi maalumu.
Wanachama wa kikundi hicho wameeleza kuwa kufanikisha upatikanaji wa mkopo huo kumetokana na jitihada za Mbunge wa Jimbo la Busanda, Dkt. Jafari Rajabu Seif, pamoja na Diwani wa Kata ya Bukoli, Faraji Seif, ambao wameendelea kuwaunganisha vijana na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotolewa na serikali.
Akizungumza wakati wa kukabidhi pikipiki hizo, Diwani wa Kata ya Bukoli, Faraji Seif, amesema mpango huo ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwawezesha vijana kujitegemea kiuchumi kupitia mikopo isiyo na riba.

Aidha, aliwahimiza vijana wengine kujiunga katika vikundi vinavyotambulika ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali za mikopo zinazotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi ya wananchi.