Latest Posts

IPPDR YAWANOA WASHIRIKI 30, MLAWA ACHANGIA MILIONI 1 AKISISITIZA MAFUNZO YAFIKE IRINGA

Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Sera za Umma na Diplomasia (IPPDR) imehitimisha mafunzo ya Itifaki na Diplomasia kwa washiriki 30 jijini Dar es Salaam, huku mgeni rasmi, mfanyabiashara Aidan Mlawa, akichangia shilingi milioni moja na kuomba mafunzo hayo yapelekwe Mkoa wa Iringa ili wananchi wengi zaidi wanufaike.

Mafunzo hayo yamewakutanisha vijana na viongozi wa umma kwa lengo la kuwajengea uwezo katika masuala ya itifaki, maadili ya kidiplomasia na uongozi unaozingatia misingi ya taaluma na weledi katika utendaji wa umma.

Washiriki walipatiwa maarifa kuhusu miiko na maadili ya kidiplomasia (Diplomatic Etiquette) pamoja na usimamizi bora wa itifaki katika uongozi (Leadership Excellence in Protocol Management), yakilenga kuimarisha ustaarabu, nidhamu na ubora wa huduma katika taasisi na ofisi mbalimbali.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mlawa alisema elimu ya itifaki ni nyenzo muhimu ya kujenga viongozi wenye maadili, nidhamu na uwezo wa kuiwakilisha Tanzania kwa weledi katika ngazi mbalimbali.

Aidha amesisitiza umuhimu wa kuyasogeza mafunzo hayo katika mikoa mingine, akitoa kipaumbele kwa Mkoa wa Iringa.

Mbali na kutoa wito huo, Bw. Mlawa alichangia shilingi milioni moja kwa ajili ya maandalizi ya mafunzo yajayo na baadaye kuwatunuku vyeti washiriki wote 30 waliofanikiwa kuhitimu mafunzo hayo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa IPPDR Tanzania, Lugano Daud Kalinga, amemshukuru Mlawa kwa kukubali kuwa mgeni rasmi, kutoa mchango wa kifedha na kuendelea kuunga mkono juhudi za kuendeleza mafunzo ya itifaki na diplomasia nchini.

Pia Kalinga aliwashukuru washiriki kwa kujitokeza kwa wingi na kumpongeza mkufunzi mwenza, Bw. Martin Kikuli, Msaidizi wa Mwakilishi wa UNESCO nchini Tanzania, kwa mchango wake katika kufanikisha mafunzo hayo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!