Latest Posts

JUBILEE YA MIAKA 100: TOSAMAGANGA YALENGA KUKUSANYA FEDHA KUKARABATI SHULE

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta amezindua maandalizi ya maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 100 ya Shule ya Sekondari Tosamaganga, sambamba na kampeni ya kuchangisha Shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule na kununua basi jipya la wanafunzi.

Akizindua kampeni hiyo Agosti 3, 2026, Sitta amesema maadhimisho hayo si ya kuadhimisha historia pekee, bali ni fursa ya kuanzisha miradi ya maendeleo itakayonufaisha wanafunzi wa sasa na vizazi vijavyo, kutoa wito kwa wahitimu (Alumni), taasisi, kampuni binafsi na wadau wengine kushiriki kufanikisha lengo hilo.

Amesema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1926 imeendelea kuwa nguzo ya elimu bora, maadili na uongozi nchini, huku kaulimbiu ya Jubilee ya mwaka huu ikisema, “Miaka 100 ya Elimu Bora, Maadili na Uongozi wa Kuigwa.”

Kwa mujibu wa Kamati ya Jubilee, fedha zitakazopatikana zitatumika kukarabati majengo yaliyochakaa, kuboresha mabweni, kununua samani, kupata basi jipya la wanafunzi na kutekeleza miradi mingine ya maendeleo kulingana na mahitaji ya shule.

Ratiba ya maadhimisho itaanza Oktoba 8 kwa matembezi ya Jubilee na shughuli za usafi wa mazingira, ikifuatiwa na mbio za Fun Run Oktoba 9 zitakazowakutanisha wahitimu, wanafunzi na wananchi.

Kilele cha maadhimisho kitafanyika Oktoba 10 na kitahusisha maonesho ya historia ya shule, nyaraka na kumbukumbu zake, utoaji wa tuzo za heshima pamoja na shughuli mbalimbali za kijamii zitakazowakutanisha viongozi wa Serikali, wahitimu na wadau wa maendeleo.

Akizungumza kwa niaba ya wahitimu wa zamani, Edward Nzalalila amesema Jubilee hiyo ni fursa ya kuirejeshea shule mchango wake kwa kuwa imezalisha viongozi na wataalamu wengi waliohudumia Taifa, akisisitiza umuhimu wa kila mdau kuchangia kuboresha miundombinu yake.

Naye mwakilishi wa Alumni, Iddy Mwerangi, amesema wadau wamepewa nafasi ya kuchagua miradi wanayotaka kuifadhili, ikiwemo ukarabati wa mabweni, maabara, ununuzi wa samani na maboresho mengine kulingana na uwezo wao.

Mwerangi amesema Alumni wamejipanga kuhakikisha shule inapata basi jipya la wanafunzi lenye thamani ya takribani Shilingi milioni 150, likiwa sehemu ya urithi wa maadhimisho ya miaka 100 ya Shule ya Sekondari Tosamaganga.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!