Serikali imevitaka vyama vya wafanyakazi nchini kuendelea kuimarisha demokrasia ya ndani, kuzingatia sheria na kuendeleza majadiliano ya kijamii ili kuimarisha mahusiano ya kazi na kuongeza tija.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi, Dkt. Eveline Munisi, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Saba wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) uliofanyika mkoani Iringa.
Dkt. Munisi aliipongeza TUICO kwa kutimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1995, akisema mafanikio hayo yanaonesha uimara wa chama na mchango wake katika maendeleo ya sekta ya kazi nchini.

Alisisitiza kuwa demokrasia, uwazi na uwajibikaji ni msingi wa uongozi bora, huku akiwataka viongozi watakaochaguliwa kuheshimu Katiba, kusimamia vyema rasilimali za chama na kuwatumikia wanachama wote bila makundi.
Aidha, alisema Serikali itaendelea kuimarisha mfumo wa utatu na majadiliano ya kijamii, akisisitiza kuwa migogoro ya kazi inapaswa kutatuliwa kupitia mazungumzo ya pamoja.
Naibu Waziri pia aliipongeza TUICO kwa juhudi zake katika kufanikisha Mikataba ya Hali Bora za Kazi na kuitaka kuongeza kasi ili wafanyakazi wengi zaidi wanufaike na mikataba hiyo.

Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kulinda haki ya wafanyakazi kujiunga na vyama vyao na kuchukua hatua dhidi ya waajiri watakaokiuka sheria za kazi, huku akisisitiza kuwa waajiri na wafanyakazi ni washirika muhimu katika maendeleo ya uchumi.
Kwa upande wake, TUICO ilisema chama hicho kimeongeza wanachama kutoka 32,000 hadi takribani 150,000 katika kipindi cha miaka 30, na kupitia mkutano huo kinachagua viongozi wapya watakaoongoza chama kwa miaka mitano ijayo.