Latest Posts

MKUTANO WA RAIS NA WAPINZANI, WAOMBA KUPEWA FURSA YA KUSAFIRI NA RAIS NJE YA NCHI, RAIS ARIDHIA

Katika hatua ya kuimarisha ukomavu na maridhiano ya kisiasa na ushirikishaji nchini, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amekubali ombi la viongozi wa vyama vya upinzani la kuambatana naye katika safari zake za nje ya nchi. Hatua hiyo imepokelewa kwa furaha na wadau wa siasa kama kielelezo cha nia ya dhati ya serikali katika kujenga maridhiano.

Uamuzi huu unatokana na kikao maalum kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam tarehe 30 Julai, 2026, ambapo Rais Samia alizungumza na viongozi wa vyama vya siasa nchini. Katika kikao hicho, viongozi wa vyama na taasisi za kisiasa walimuomba Rais kukubali utaratibu huo ili kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kuwapa fursa viongozi wa vyama hivyo kujifunza mengi nje ya nchi kwa mustakabali wa taifa la Tanzania.

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatibu, ameithibitishia Jambo TV kuwa utekelezaji wa uamuzi huo ulianza katika safari ya hivi karibuni ya kwenda nchini Angola. Viongozi walioteuliwa kuandamana na Rais katika safari hiyo walikuwa ni Juma Ali Khatibu mwenyewe (kutoka chama cha ADA-TADEA) na Dorothy Semu ambaye ni Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo.

Hata hivyo, wakati Juma Ali Khatibu akishiriki safari hiyo, Dorothy Semu hakufanikiwa kwenda. Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake wa Chama cha Wakulima (AAFP) Taifa, Shani Ally Kitumbua amedai kuwa Semu alitafutwa sana kwa njia ya simu bila mafanikio licha ya kuwa vigezo vya safari hiyo vilikuwa vimekamilika.

Akizungumza na wanahabari Agosti 5, 2026, Kitumbua alionya kuwa kitendo hicho kinaweza kumvunja nguvu Rais ambaye ameonesha nia ya kuwashirikisha wapinzani.

Hata hivyo, katika mahojiano na Jambo TV kuhusu tukio hilo, Dorothy Semu amegoma kutoa maelezo ya kina au sababu za yeye kutoshiriki safari hiyo akisema “no comment”.

Pamoja na changamoto hiyo iliyojitokeza katika safari hiyo, Baraza la Vyama vya Siasa limempongeza Rais Samia kwa utaratibu wa kukutana na vyama vya siasa mara tatu kwa mwaka na kuwashirikisha katika safari za nje. Linaamini kuwa utaratibu huu utasaidia kutoa fursa kwa viongozi wa upinzani kujifunza na kutoa mchango wao katika diplomasia ya nchi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!