Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ametoa ufafanuzi kuhusu matukio ya ghasia yaliyotokea nchini mnamo Oktoba 29,2025 akidai kuwa yalikuwa na ajenda maalum ya siri na hayakufanyika kwa utashi wa hiari wa Watanzania wengi.
Katika mahojiano maalum na shirika la habari la DW, Katambi amebainisha kuwa ushahidi upo wazi kuwa machafuko hayo yalipangwa na kuratibiwa kwa malengo ya kisiasa. Waziri Katambi amewataka Watanzania na jumuiya ya kimataifa kujiuliza maswali ya msingi kuhusu uhalali wa kile kilichoitwa maandamano siku hiyo. Amehoji ni nchi gani duniani inayoruhusu maandamano siku ya uchaguzi mkuu, na ni sheria gani inayoruhusu maandamano yasiyokuwa na taarifa, viongozi wanaojulikana, wala ruti maalumu.
“Nchi gani duniani imewahi kuruhusu maandamano kama yangekuwa ya halali, halafu waandamanaji wakaenda kwenye duka la simu la mtu wakachoma moto… wakaenda kwenye sheli wakachoma sheli moto… wakaenda kuchoma vituo vya polisi?” amehoji Katambi akionesha kusikitishwa na uharibifu wa miundombinu muhimu ya taifa
Katambi ametoa hoja ya kitakwimu akijiuliza kwanini ghasia hizo zilitokea katika mikoa minne au mitano tu, wakati taifa lina watu zaidi milioni 61. Amebainisha kuwa ikiwa hasira ingekuwa ya wananchi wote, ghasia hizo zingejitokeza pia vijijini ambako asilimia 70 ya Watanzania wanaishi, lakini hali huko ilikuwa ya utulivu
Aidha, amewashutumu aliowaita viongozi wa maandamano hayo kwa kushindwa kujitokeza tarehe 30 au 31 Oktoba kuomba radhi kwa mali zilizopotea, badala yake wakaendelea na uchochezi.
“Wakati haya yanatokea na kama kweli…si ilikuwa siku tarehe 29 Oktoba, tarehe 30 kwanini hawakujitokeza viongozi wa kusema kwamba sasa sisi tulikuwa tuna maandamano halali lakini imetokea bahati mbaya labda kuna wahuni waliingilia, tunaomba radhi kwa mali zilizopotea kwa wale waliofanyiwa uhalifu, kwanini, tarehe 30. Kwanini hawakujitokeza hao viongozi? Tarehe 31 sijui tarehe moja, kwanini badala ya kusikia watu wakitoa kauli za pole kwa mamlaka mbalimbali na walioathirika badala yake tulisikia uchochezi wa aina nyingine, na baadhi ya watu kujilaumu kwamba tumefeli tungefanya hivi…tarehe moja, kwanini hatukuona hata baadhi ya viongozi wa dini wakitoka kukemea kwamba lilofanyika ni baya, baadhi of course walisema, baadhi ya viongozi walisema wa dini lakini kuna wengine wengine waliamua kukaa kimya. Hatukuona viongozi wa kisiasa wakijitokeza pia kuonesha upande wao kwamba wamefurahishwa au wamekasirishwa”, amehoji Katambi.
Waziri huyo amehoji pia kwanini kulikuwa na jitihada kubwa za kuipinga Tume ya Jaji Chande iliyoundwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema kuwa kupinga tume hiyo ni kupinga hatua za kisheria zinazotambuliwa kimataifa.
“Sheria za kimataifa lazima mchukue sharia, mchukuliane hatua kwa mujibu wa sheria zilizopo kwanini tume imeundwa wakaanza ku-challenge kwa nia hiyo njema? kwanini baada ya kuona wameshindwa kuvunja uhalali wa tume wakaanza kuwapinga wajumbe wa tume kwamba sio halali?… walivyoona wajumbe wa tume ni imara na wana uwezo na wana ‘credibility’ na heshima kubwa kimataifa wakaamua kwenda kupinga matokeo ya tume? Kwanini wanapinga matokeo ya tume?… Na kwanini wanapinga matokeo ya tume, kwa utafiti gani wao walioufanya na kwa idadi ipi? Walitaka Watanzania wafe zaidi ya wale? amehoji Katambi akijibu madai ya wanaosema idadi ya vifo ilikuwa ndogo.